Thursday, July 30, 2009

Kiwanda cha Bia Dar chawaka moto.

Moto mkubwa uliolipuka usiku wa kuamkia jana katika Kampuni ya Bia Tanzania Breweries (TBL), umeteketeza mali mbalimbali zikiwamo kreti zenye chupa zaidi ya 200,000 zinazokadiriwa kuwa na thamani ya Sh2.4 bilioni.

Moto huo ulioanza saa saba usiku ulisababisha moshi mzito kuzagaa katika maeneo ya Ilala-Boma, Mchikichini na Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Watu wanaoishi katika baadhi ya mitaa ya Ilala na hasa karibu na kiwanda hicho walitaharuki na kuzikimbia nyumba zao huku vilio vikisikika kila kona baada ya moto mkubwa kuzuka katika kiwanda hicho.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TBL na kusainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Robin Goetzsche, chanzo cha moto huo bado hakijajulikana ingawa taarifa za awali zinaeleza kuwa moto huo ulisababishwa na hitilafu ya umeme.

Taarifa hiyo ilisema moto huo ulizibitiwa majira ya saa tisa za alfajiri kwa ushirikiano wa Kikosi cha Zimamoto cha Jiji, Ultimate Security Fire Services, Knight Support, Tanzania Ports Authority pamoja na Tanesco kuzima umeme unaoingia kiwandani humo.
Taaarifa hiyo ilisema moto huo ulizuka katika eneo la kuhifadhia chupa tupu na iliwaondoa hofu wateja wake na kwamba, kiwanda hicho kitaendelea na uzalishaji na kutoa huduma yake kama kawaida.


Wananchi wanaoishi jirani na kiwanda hicho waliamshwa na kelele za chupa zilizokuwa zikiungua huku watu wasiojulikana wakipita katika nyumba za watu kuwaamsha.
Hofu ya wananchi hao wanaoishi karibu kabisa na kiwanda hicho iliwafanya wazihame nyumba zao na kukimbilia mbali na eneo hilo kwa kuogopa madhara ya moto huo.


Wakati wananchi hao wakikimbia nyumba zao, baadhi ya wananchi kutoka maeneo ya jirani walikuwa wanasogelea eneo la kiwanda hicho ingawa hawakusogea karibu na sehemu iliyokuwa ikiwaka kutokana na moto kuwa mkubwa.
Licha ya Mtaa wa Mchikichini kilipo kiwanda hicho kusifika kuwa na vibaka wengi, hawakuweza kuingia katika kiwanda hicho kufanya uhalifu kwa hofu ya kudhuriwa na moto huo pamoja na ulinzi mkali uliokuwepo.


Askari kanzu na waliokuwa wamevaa sare na bunduki walikuwa wamejaa katika eneo hilo kuimarisha usalama wa raia na mali zao na kiwanda hicho.
Ingawa vikosi vya zimamoto vilifanikiwa kuudhibiti moto huo jana alfajiri, moshi uliendelea kuwepo katika eneo hilo kutokana na kuungua kwa kiasi kikubwa cha kreti za kubeba bia pamoja na chupa zake.


Maeneo yanayozunguka kiwanda hicho yalikumbwa na giza ghafla baada ya kuzuka kwa moto huo na kusababisha nguzo na nyaya za umeme zilizopo katika eneo kuteketea kwa moto.
Wananchi wengi walikuwa na hofu ya madhara zaidi kutokea endapo mitungi ya gesi iliyopo kiwandani hapo ingefikiwa na moto huo.

Hata hivyo, vikosi vya zimamoto vilifanikiwa kudhibiti moto huo kabla haujafika mahali mitungi hiyo ilipokuwa imehifadhiwa.
Jana saa 6:00 mchana ripota wetu alishuhudia askari wa kikosi cha zimamoto wakiendelea kuudhibiti moto uliokuwa ukiendelea kuwaka mahali zilipokuwa zimehifadhiwa kreti za bia zizoteketezwa.

1 comment:

  1. Pole Tanzania kwa ajali hii kubwa. Na pia pole sana wanywaji wa bia.

    ReplyDelete