Friday, April 23, 2010

Mzee Mtei amtabiria anguko Rais Kikwete

Mwanasiasa mkongwe nchini Edwin Mtei amemtabiria mabaya Rais Jakaya Kikwete kuwa atakabiliwa na upinzani mkali katika uchaguzi mkuu ujao tofauti na chama chake kinavyodhani.
"CCM itakabiliwa na upinzani mkali wakati wa uchaguzi mkuu tofauti na viongozi wake wanavyodhani. Hata Rais, Kikwete naye atakumbana na upinzani mkali tofauti na ushindi alioupata mwaka 2005," alisema Mtei.
Alisema matumaini ya CCM na Kikwete kuwa watapata ushindi kiurahisi ni ndoto, kwani wakabiliwa na ushindani mkubwa kutokana na wananchi kuchoshwa na utendaji mbovu wa chama hicho juu ya ahadi walizotoa mwaka 2005 ambazo hazijatekelezwa.
Kuhusu hatua ya CCM kuchangisha fedha kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao, Mtei ambaye pia ni muasisi wa Chadema alisema wameiga kutoka Chadema, kwa sababu sera za CCM haziwezi kuvutia wananchi.
Mtei ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Fedha na Gavana wa Benki Kuu alisema mkakati huo uliozinduliwa na Rais Jakaya Kikwete, hauwezi kuwavutia wala kuwashawishi wananchi kuichangia CCM na kuwa haina jipya.
"Nawaonea huruma CCM, kwani hawana jipya, hawawezi kubuni kitu kipya cha kwao. Sisi tulianza kuchangia fedha kwa njia ya uwazi na wao wamefuata nyayo; kwa kweli CCM hawana jipya,"alisema Mtei
"Sera za CCM kamwe haziwezi kuwavutia wananchi hadi wakichangie chama hicho, serikali inadai inapiga vita ufisadi, wakati serikali hiyo hiyo imeshindwa kuwadhibiti mafisadi na wahujumu uchumi walio ndani ya chama chao,"alisiitiza Mtei.
Akizungumzia fedha za Mfuko wa Kichocheo cha Maendeleo ya Jimbo(CDCF) zinazotarajiwa kugawanywa mwishoni mwa mwezi huu, Mtei alisema fedha hizo zitaangukia kwenye matumizi ya siasa badala ya mandeleo ya majimbo kama ilivyokusudiwa.
"Huwezi kutoa pesa kipindi hiki, hizi ndizo siasa za nchi hii. Hizi pesa za mfuko wa kichocheo cha maendeleo ya jimbo ni za siasa si za maendeleo, kwani hazina jipya,"alisema Mtei bila kufafanua.

No comments:

Post a Comment