Thursday, January 13, 2011

Je, kikwete ni saafiii?

Sijui kwanini tunazungushana na kudai watu wote walioatajwa kwenye orodha ya Ufisadi wanastahili isipokuwa Rais Kikwete! Hata viongozi wanaotambua baadhi ya uzito wa tuhuma zilizotolewa na wanaodai kuwa zitiliwe maanani hujikuta wanajing'ata ng'ata kuhusu Rais Kikwete. Baadhi ya watu wamefikia mahali pa kulaumu kina Dr. Slaa kumuweka Kikwete katika kundi hilo kwani JK ni safi! Hata hivyo ushahidi wote uliopo unaonesha kuwa JK siyo safi na yeye ndiyo awe wa kwanza kujibu tuhuma zilizoelekezwa kwake!

a. Mkataba wa IPTL ulisainiwa yeye akiwa Waziri wa Nishati na Madini. Hakuna mkataba mbovu kama huo. Kushindwa kwake kutetea maslahi ya nchi akiwa Waziri na kulisababishia Taifa hasara kubwa ilikuwa ni kilele cha kutokuwajibika na kushindwa kuongoza. Akiwa Waziri mwenye dhamana ya nishati Ndg. Kikwete alitakiwa kuhakikisha kuwa serikali ya Jamhuri ya Muungano inaingia kwenye mkataba ambayo inaweza kujitoa pasipo kupata adhabu kubwa. Alishindwa na hivyo kuoneshea kutokuweza kusimamia maslahi ya nchi.

b. Wakati Rada ya bilioni 50 inanunuliwa, Ndg. Kikwete alikuwa ni Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Uhusiano wa Kimataifa na wakati sakata lenyewe linaanza alikuwa ni Waziri wa Fedha. Akiwa Waziri mwenye dhamana hiyo alishindwa kabisa kufuatilia ukweli kuwa kampuni ya BAE siyo mali ya serikali ya Uingereza na ya kuwa rada yenyewe ilikuwa imeongezwa kwa asilimia 24. Kiasi hicho kinakaribiana kabisa na wastani wa asilimia 20 za fedha za umma zinazopotea katika manunuzi ya serikali (public procurement).

Alishindwa kuhakikisha kuwa maslahi ya Taifa letu yanalindwa na alipopata nafasi ya kuonesha busara aling'aka na kusema "kwanini sisi ni idara ya Benki ya Dunia? ni kututukana kudai kuwa tusubiri Benki ya Dunia kutuamulia nini kinatufaa".

Ndio maana leo hii anapokuja na kuzungumza kuwa hawezi kuamini kuwa nchi kama Uingereza inaweza kuacha kampuni "yake" kurusha rada hiyo kwa bei hiyo wengine tunamshangaa kwani alikuwa na nafasi zaidi ya 20 ya kuweza kupinga ununuzi huo lakini alikuwa ni kinara wa kutetea tenda hiyo ya rushwa! Ni kuelewa hilo ndio utaona ni kwanini hakutaka watu wamuulize Rais Mkapa juu ya suala la rada, kwani miongoni mwa wahusika wakubwa ni yeye mwenyewe Kikwete.

c. Kama nilivyoonesha hapo juu kuwa Rais Kikwete aliwahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini. Kwa hivyo nina uhakika kabisa alikuwa anajua kabisa jinsi mikataba inavyoingiwa na alikuwa na kila sababu ya kuhakikisha kuwa mikataba inalinda maslahi ya nchi na kunufaisha nchi wakati inawapatia wawekezaji faida ya kibiashara. Kwa kitendo chake yeye mwenyewe kuwa ukaribu na wafanyabiashara hao hasa swahiba wake ambaye ni mmiliki mkubwa wa ardhi yenye vito na madini Bw. James Sinclair, Rais Kikwete tangu akiwa Waziri wa Nishati na Madini na baadaye Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje amekuwa mtu aliyetiwa upofu na "dhahabu".

Wakati Rais Mkapa na Yona wanajipatia tenda ya Kiwira, Rais Kikwete na Msabaha walikuwa wanajisogeza karibu na Kampuni ya Tanzania Royalty Exploration ambapo kuna madai kuwa Msabaha na Kikwete walikuwa na "hisa" za kiasi fulani. Kampuni hiyo ya TRE iliingia mkataba na Barrick Gold kuwa inapovumbua madini katika ardhi inayomiliki basi Barrick wanakuwa wanunuaji wa kwanza.

Ni wao TRE waliouzia Buzwagi kwa Barrick na maeneo mengine kadhaa kwa makampuni mengine. TRE inaponufaika kwa mikataba mibovu ambayo serikali inaingia na makampuni ya uchimbaji kuna watanzania wawili ambao nao wananufaika (ni wazi wapo wengine wengi na ni vigogo) na dili hizo.

Ni kwanini Barrick walikuwa wa kwanza kukubali mabadiliko ya vipengele vya mikataba yao? jibu ni ushawishi wa James Sinclair na Kikwete ili kutetea kilicho chao. Kwa yale makampuni ambayo hayana ukaribu wa James Sinclair na Kikwete (JK alimualika JS kwenye kuapishwa kwake na mara nyingi amekuwa mgeni wake akija US, na binti ya JS aliyeko Tanzania ni rafiki wa karibu) basi imekuwa vigumu kuwashawishi kubadili vipengele hivyo.

Ndio maana hadi leo hii si kweli kuwa kupitia vipengele na kuzungumza na "wakubwa" hao kuhusu mikataba kumekoma kama alivyodai mjasiriamali mwingine Nazir Karamagi alipokuwa akijaribu kupangua hoja za Zitto. Ukweli ni kwamba kamba waliitundika wenyewe serikali na ni wenyewe walioziweka shingo zao humo! wawekezaji wanatishia kuondoa kigoda!! Serikali inabembeleza!

Anapozungumzia matatizo ya mikataba Rais Kikwete anazungumzia kana kwamba tatizo ni kipengele kimoja tu! Hajachukua muda kufuatilia uzito wa hoja hizo kwani kwake ni kelele!

d. Kikwete si Safi kwani amewalinda watu wachafu! Waswahili walisema ukiwa na urafiki na wezi, usishangae watu wakakuhisi na wewe mwizi! Rais Mkapa anapomlinda mjasiriamali Mkapa, aliposhindwa kumsimamisha kazi mara moja Ditto na kuamua kumuacha ajiuzulu huku akiendelea kupata mafao yake alionesha udhaifu mkubwa wa uongozi!

Rais Kikwete amekuwa mtetezi wa wabadhirifu akikesha kutoa vitisho hewa akijaribu kutetemesha mabua na kuangusha vichuguu huku milima ikiendelea kuganda theluji! Ukimya wake kama ule wa Mkapa ni ishara wazi kuwa walifeli darasa la Mwalimu!

Anapoona kuwa madai ya ubadhirifu Benki Kuu, matumizi mabaya ya madaraka, ubadhirifu, n.k kuwa "kelele za upinzani" na kuwa "ndiyo demokrasia" anaonesha udhaifu mkubwa usiomstahili kiongozi wa nchi. Haiwezekani upotevu wa mabilioni ya fedha, matumizi mabaya ya madaraka kuwa viwe ni "kelele" tu!

Rais ni lazima we mtu ambaye hapuuzii masuala mazito na hayafanyi kuwa ni ya kijinga. Kwa mtu kuwa mpinzani hakuifanyi hoja yake kuwa "kelele". Leo hii wana CCM wenzake wanazungumza wazi kuhusu tuhuma hizi na kudai kuwa wanaotuhumiwa (akiwemo yeye mwenyewe) wajibu siyo suala la kupuuzia!

e. Rais Kikwete ameonesha na anaendelea kuonesha udhaifu mkubwa wa maamuzi hasa kwa kuwa mtu wa kusita sita na ambaye yuko tayari kutumia uwezo wake wote kutofanya lolote. Hivi hadi nini kitokee ndipo Rais Kikwete atajua kuwa mambo haya si ya kupuuzia? Wakati Lowassa ameenda kukutana na Karamagi kule London na mkataba wa Buzwagi ukasainiwa je Rais Kikwete alifahamu ujio wa Waziri wake Mkuu? Je walikutana? Kama Rais hakujulishwa kutiwa saini kwa mkataba mkubwa namna hiyo na Waziri Mkuu anakutana na Waziri mwingine pasipo ujuzi wa Rais je haoni ni ukosefu mkubwa wa kiutawala!? Lowassa alifuata nini London na kukutana na Karamagi badala ya kukutana na Rais?

Leo hii watu wakihoji mazingira ya kusainiwa mkataba huo kwanini hiyo iitwe kelele!

Tanzania imefanya kosa kubwa kumchagua Kikwete. Kosa hilo vizazi vijavyo vitasimulia kama hadithi, kuwa "hapo zamani za kale kulikuwa na mwana CCM mmoja ambaye aliwapo watu matumaini sana kabla ya uchaguzi. Watu wengi waliamini kuwa mwanaCCM huyo ndiye atakuwa mkombozi na kiongozi wa kuwaonesha njia ya kufikia nchi ile ya ahadi. Walipomchagua kwa asilimia 80 ya wapiga kura, Watanzania walijawa na matumaini... Miaka miwili baadaye watanzania walishika vichwa vyao kujuta, kwani waliyemdhania ndiye kumbe siye... !! "....

Kama Rais Kikwete hatabadili mwelekeo wa uongozi wake, na kama ataendelea kufanya kazi kana kwamba madai na hoja zinazojengwa ni "kelele" tu na hivyo kuendelea kufumba macho ufisadi unaoendelea nchini (na hapa simaanishi rushwa ya kutoa na kupokea tu, namaanisha matumizi mabaya ya madaraka, n.k).

1 comment: