Saturday, May 7, 2016

sakata la uhaba wa sukari nchini

Mfanyabiashara mmoja amekamatwa na tani 4,900 za sukari Mbagala, Dar es salaam na kikosi kazi kilichoundwa kufanya upekuzi. 
Inasadikiwa kuwa wafanyabiashara wa bidhaa hiyo wamekuwa sio waaminifu na kuficha bidhaa hiyo muhimu kwa jamii baada ya serikali kutoa maelekezo kwa wafanyabiashara hao kuwa wanapaswa kuuza bidhaa hiyo kwa bei elekezi ya shilingi 1800 kwa kilo.

Pekua pekua hiyo imeanza mara baada ya rais kutoa Dkt John Magufuli kutoa tamko la kufanya msako nchi nzima kubaini wafanyabiashara wasio waaminifu walioficha bidhaa hiyo katika kuonyesha kupinga kwao kuuza bidhaa kwa kutumia bei elekezi iliyotolewa na serikali. 
Wafanyabiashara watakaobainika kutenda kosa hilo watakabiliwa na aidha faini kali,kushitakiwa mahakamani ama kufutiwa leseni zao za biashara.Monday, June 3, 2013

CHADEMA yaitaka serikali kuacha kuibambikia kesi

Dk. Willibrod Slaa,Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),amemtaka Rais Jakaya Kikwete na chama chake waache kuwabambikizia kesi za ugaidi na uchochezi wapinzani.


Dk. Slaa alisema hata kama viongozi na wanachama wa CHADEMA wataendelea kubambikiwa kesi hawatoacha kupambana na CCM hadi chama hicho kitakapoondoka madarakani.

Kauli hiyo aliitoa juzi katika viwanja vya Uwanja wa Ndege mjini Morogoro alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara ambapo alisema wanaamini Rais Kikwete ameshindwa kuisimamia serikali yake.

Alisema kushindwa huko kwa Rais ndiko kunakomfanya kila kukicha kutafuta makosa ya kuwabambikia wapinzani wanaoupinga utawala wake mbovu.

“Tutaendelea kupambana na serikali ya Kikwete kwa njia yoyote hadi itakapoondoka,nyie tubambikezieni kesi za ugaidi, uchochezi na nyingine za kusingiziwa lakini hatutakubali watoto wa baadaye wachezewe kwenye mambo nyeti kama elimu,” alisema.

Alisema serikali ya CCM imeshindwa kusimamia uongozi bora tangu miaka ya 1990 kwa kuondoa misingi ya utawala na kuingiza misingi mibovu inayolita hasara taifa na wananchi wake kwa kujineemesha watawala peke yao.

Alibainisha kuwa watawala sasa  hivi wanaichezea nchi kwa kutoa vituko vya kila aina ikiwemo cha hivi karibuni ambapo serikali ilifuta matokeo ya kidato cha nne 2012 na kuyapitia upya.

Aliongeza kuwa pamoja na kuyapitia upya bado idadi kubwa ya wanafunzi wamefeli mitihani hivyo CHADEMA haitokubali CCM iendelee kuharibu taifa na kizazi kijacho.

Alisema hawezi kufanya unafiki wa kwenda kwenye majumba ya ibada kuomba amani kama wafanyavyo viongozi wengine kwa shinikizo la Rais Jakaya Kikwete wakati Watanzania wanataabika kwa utawala mbovu.

Alibainisha kuwa Watanzania wanakabiliwa na matatizo mengi yakiwemo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa ambayo ni chanzo cha kutoweka kwa amani.

Alisema Kikwete na serikali yake bado hawajayaelewa au wanayapuuzia matatizo yanayochangia kuvurugika kwa amani.

Dk. Slaa alitoa mfano wa migogoro ya ardhi inayoikumba mkoa wa Morogoro kila mara inasababishwa na ufinyu wa uadilifu kwa watumishi wa serikali ambao ni matunda ya serikali ya CCM.

“Amani haihubiriwi ikaja au ikaimarika, hujengwa na kuimarishwa kwa misingi bora na uadilifu katika uongozi wa nchi ambao sasa haupo,” alisema.

“Sitaki unafiki wa kwenda eti kuombea amani, amani ipi? leo kuna taarifa za kila aina juu ya uovu ikiwemo wizi wa rasilimali za nchi, wananchi wakiendelea kutaabika na ugumu wa maisha kila kukicha lakini serikali imekaa kimya.”

Awali kabla ya Dk. Slaa kuhutubia Mwenyekiti wa Baraza la Vijana CHADEMA (BAVICHA) John Heche aliwataka wananchi wabadilike kwa kuiondoa CCM madarakani ili wapate maisha bora.

Alisema watawala wanajifanyia watavyo kwa kujichukulia rasilimali zilizomo nchini kwa manufaa yao kwa sababu ya kujiamini wataendelea kutawala milele.

“Nchi hii ili iendelee inahitaji utawala ubadilike na wa kuubadili ni ninyi wananchi...’ipigeni’ chini CCM 2014 na 2015 na kutuweka sisi tukishindwa kutekeleza tuliyokubaliana na ‘tupigeni’ chini wekeni chama kingine chochote,” alisema.

Wednesday, May 29, 2013

Spika makinda, azima hoja ya wapinzani kuhusu umiliki wa ardhiSpika wa Bunge, Anne Makinda jana aliizima hoja ya Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee kuhusu umiliki wa mashamba makubwa yasiyoendelezwa wakati wa kujadili hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambayo ilihitimishwa bungeni jana.
Mdee alivutana na Spika Makinda wakati wa kujadili bajeti hiyo kifungu kwa kifungu, Mdee alitaka kufahamu kauli ya Serikali kuhusu kampuni zinazomiliki ardhi bila kuziendeleza na hatua zinazochukua kuhakikisha zinarudishwa kwa wananchi.
Baada ya kuuliza swali hilo huku akisisitiza kutoa shilingi, Spika Makinda alimtaka kukaa chini kwa kuwa hoja yake haina mashiko ya kufanya hivyo.
 “Kaa chini, nakwambia kaa chini,” alisema Makinda huku Mdee akionekana kuendelea kuzungumza... “Nasema kaa chini,” alirudia na Mdee kukaa huku akikipeperusha karatasi hewani kuonyesha kutokubaliana naye.
Awali, Mdee alisema shamba la Simanjiro ambalo Halmashauri ya wilaya hiyo ilipendekeza mwekezaji kupewa ekari 500 lakini Wizara ya Ardhi iliidhinisha ekari 25,000 ambazo mwekezaji hajaziendeleza zote wakati mashamba ya Kisarawe na mashamba ya mkonge Tanga ambayo wawekezaji wameyakopea fedha nayo hadi sasa hayajaendelezwa.
Alitaka kauli ya Serikali kuhusiana na hali hiyo na jinsi ya kurudisha mashamba hayo katika miliki ya umma. Mbunge mwingine aliyetishia kutoa shilingi ni Dk Faustine Ndungulile wa Kigamboni (CCM), akijikita katika suala la ujenzi wa mji mpya wa Kigamboni akisema wananchi wake hawakushirikishwa katika mipango ya ujenzi huo.

Tuesday, May 28, 2013

Suala la Mtwara ni zaidi ya Gesi asilia - Kutumia nguvu ya dola sio njia pekee ya Amani - Zitto Kabwe

Serikali iangalie upya namna inavyolitazama suala la Mtwara. Hivi sasa suala hili linaonekana kiusalama zaidi badala ya kuliona kama suala la kijamii na maendeleo lenye kuhitaji kujenga imani ya wananchi.

Suala hili linahitaji muda na heshima kwa wananchi. Ni vema tuache sauti ya wananchi kusikika na kuzitolea maamuzi sahihi yenye kujenga kuaminiana na kuheshimiana kati ya dola na wananchi.

Suala la Mtwara ni zaidi ya gesi asilia. Ni matokeo ya kutengwa kimaendeleo kwa muda mrefu. Suala la Gesi ni nafasi ya kuunganisha watu wa kusini na Jamhuri ya Muungano. Tuamue sasa kufanya maamuzi sahihi na kuunganisha Jamhuri yetu au kukosea na kudharau na kuivunja Jamhuri yetu.

Kama Kuna mataifa ya kigeni/makampuni binafsi yanahusika na hali ya Mtwara. Serikali iyataje mataifa hayo na makampuni hayo hadharani na vibaraka wao.Vinginevyo nadharia hizi zitaonekana ni propaganda tu kwa lengo la kufunika kombe mwanaharamu apite.

Nadharia zote za kuelezea masuala ya Mtwara zinakimbia suala la msingi la  kutengwa kwa muda mrefu sana kwa mikoa ya kusini kwenye maendeleo ya nchi. Ahadi za Rais Ben Mkapa kuhusu Mtwara Corridor, ahadi za Rais Jakaya Kikwete za 2005 na biashara ya korosho ni miongoni mwa malalamiko ya muda mrefu ya wananchi wa Mtwara. Suala hili la msingi lazima lipatiwe majawabu muafaka kwa maelezo yenye heshima kwa wananchi badala ya dharau na vijembe dhidi ya raia.

Kuna kukosa imani kukubwa kwa wananchi dhidi ya Serikali. Suala hili ni pana zaidi na linasambaa Tanzania nzima. Malalamiko yanaposhawishiwa kihofu tu huleta matatizo makubwa sana. Hali ya namna hii haijawahi kutokea nchini mwetu. Kukamata na kufunga viongozi wa wananchi haitosaidia kamwe.

Kutumia nguvu ya dola kuzima vuguvugu la wananchi sio njia pekee ya kujenga amani. Makovu ya kutumia nguvu ya dola huchukua muda mrefu sana kupona. Lazima kubadili mkakati wa kuongoza na kuliweka Taifa sawa

Hatimaye Lipumba akiri kumbeba JK mwaka 2010

     Hatimaye mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amekiri kukihusisha chama chake cha CUF na “kumnusuru” Rais Jakaya Kikwete katika uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka 2010.Profesa Lipumba alitoboa siri hiyo katika Msikiti wa Idrissa, Kariakoo, jijini Dar es Salaam, alikokwenda kuswali swala ya Ijumaa katika mojawapo ya Ijumaa za mwezi huu.


Kwa mujibu wa video ya tukio hilo iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii mapema wiki hii, Profesa Lipumba alikaribishwa kuzungumza na waumini hao mara baada ya utangulizi uliotolewa na Imamu wa msikiti huo, Sheikh Ali Basaleh, aliyemtaka awaeleze Waislamu hali ya kisiasa nchini kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2015.


Huku akisisitiza juu ya umuhimu wa mshikamano wa kiimani, Profesa Lipumba alianza kwa kuzungumzia matokeo ya uchaguzi mkuu wa 2010, na ushindani mkali wa kisiasa uliokuwapo.

Alisema hawaoni matunda ya jitihada walizofanya kumnusuru Rais Kikwete asishindwe kwa mantiki ya udini (uislamu), kwani hata chini ya uongozi wake, Waislamu wameendelea kutothaminiwa.

“Ninyi masheikh mnajua vizuri zaidi hali ya kisiasa ilivyokuwa, kwamba ilibidi zifanyike juhudi za makusudi ili kuokoa jahazi. Lakini pamoja na kuliokoa jahazi, hali halisi inaonyesha mpaka sasa hakuna matunda yoyote yaliyopatikana, na tupo katika mtihani mgumu zaidi,” alisema.

Katika hali ambayo inasemekana ushindi wa Rais Kikwete ulipatikana kwa mbinu, huku wengine wakiituhumu Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa ilimnusuru mgombea wa CCM, kauli hii ya Profesa Lipumba inadokeza kwamba anajua mkakati zaidi wa kazi ya Tume ya Uchaguzi.

Katika hali isiyo ya kawaida, Profesa Lipumba anaonekana kuhamasisha Waislamu kujipanga akisema “wenzetu wameanza kujipanga” kuelekea 2015.

“Kwahiyo kama Waislamu tunataka kupata haki zetu, kama tunataka kuishi kama raia wa daraja la kwanza katika nchi yetu, lazima tujipange kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015; na sisi tuanze kujipanga kwa sababu wenzetu wameanza kujipanga, vinginevyo tutaendelea kubaki maskini na raia wa daraja la nne katika nchi yetu wenyewe.

“Mwaka 2010 wakati mshindi wa uchaguzi wa rais alipotangazwa, mimi nilikwenda kwenye hafla ya kutangazwa matokeo, na nilikwenda makusudi tu, siyo kwamba uchaguzi ulikuwa huru na wa haki, ila nilikwenda makusudi kwa kujua hali ya kisiasa ilivyokuwa wakati huo.

“Huku nilikutana na Sheikh Basaleh. Nilipokutana naye, alinipongeza; sijui kama yeye anakumbuka, akaniambia ‘umeweka mbele imani yako na umekuwa mwelewa wa mambo.’”

Hata hivyo, licha ya Profesa Lipumba kuwaambia Waislamu wajipange kwa ajili ya uchaguzi mkuu, hakusema wajipange kupitia chama kipi.

Itakumbukwa kuwa kumekuwepo tuhuma dhidi ya Rais Kikwete na CCM kuwa mwaka 2010 waliendesha propaganda chafu za udini zenye lengo la kuwagawa Watanzania hususan Wakristo na Waislamu kwa manufaa yao ya kisiasa.

Serikali yaendelea kumbeba Jairo

Utamaduni na desturi ya  serikali ya awamu ya nne wa kutotekeleza maazimio ya Bunge kwa kuwachukulia hatua watendaji wake waliotiwa hatiani na kamati teule, huenda ukamnufaisha aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo.


Hatua hiyo ni kutokana na msimamo wa waziri wa wizara hiyo, Profesa Sospeter Muhongo, kuonyesha hayuko tayari kuchukua hatua zozote kwa Jairo aliyesimamishwa kazi kutokana na matumizi mabaya ya madaraka.

Jairo alituhumiwa kukusanya na kutumia fedha za serikali kinyume cha sheria, kanuni na taratibu za fedha za umma na kuruhusu matumizi mabaya ya fedha za umma.

Kamati teule ya Bunge iliyoundwa kuchunguza tuhuma hizo kwa kipindi cha mwaka 2011/2012, ilipendekeza serikali ichukue hatua za kinidhamu kwa Jairo.

Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni kwa Wizara ya Nishati na Madini, John Mnyika, wakati wa kuwasilisha maoni yao kwa mwaka wa fedha 2013/2014 aliitaka serikali ieleze kwa nini haikutekeleza maazimio ya Bunge.

Hata hivyo, katika kuhitimisha hoja za wabunge mwishoni mwa wiki, Waziri Muhongo aliligeuza sakata kuwa la kisiasa huku akiwashambulia CHADEMA kuwa wanafanya porojo.

“Muda wa porojo umekwisha na ndio maana mimi ukinitajia mlolongo wa kesi ukitaka nikafukue mafaili pale ofisini, mimi ni mbunge wa kuteuliwa nikapewa uwaziri nadhani hawakunituma pale kupekua mafaili,” alisema.

Muhongo alisema kwa vile CHADEMA wana ushahidi na vyombo vya dola vipo wapeleke suala hilo mahakamani.

Majibu ya waziri Muhongo yalipingwa na Mnyika wakati Bunge likiwa limekaa kama kamati kupitia kifungu kwa kifungu na kutaka apatiwe ufafanuzi wa kujitosheleza huku akitoa kusudio la kutoa shilingi kwenye mshahara wa waziri endapo asingeridhika.

Hata hivyo, kusudio la Mnyika lilitupiliwa mbali na Spika wa Bunge, Anna Makinda, ambaye alitoa muda mwingi kwa wabunge kuhoji vifungu na kisha akatumia kanuni kupisha mafungu kwa ujumla.

Akizungumzia kauli ya Muhongo, Mnyika alisema kuwa waziri huyo ni muongo na ushahidi wa kumbukumbu rasmi za Bunge (hansard) ya Julai 28 mwaka 2012 unaonyesha.

“Nilihoji kuhusu utekelezaji wa maazimio ya Bunge juu ya gesi asilia na sakata la Jairo, waziri akajibu: ‘Hafanyi kazi kwa redio na magazeti.’ Hii ni dharau kwa Bunge.

“Mwaka huu 2013 katika hotuba yangu nimehoji tena kuhusu maazimio ya Bunge ya Richmond, Kiwira, Jairo, Mpango wa Dharura wa Umeme, mafuta na gesi asilia lakini hatua hiyo ameiita porojo,” alisema.

Mnyika alisema kuwa waziri anasahau kwamba kama maazimio hayo yangetekelezwa kwa wakati nchi isingekuwa na mgogoro katika gesi asilia ikiwemo ujenzi wa bomba na pia uchumi usingeathirika kutokana na matatizo ya umeme.