Wednesday, March 18, 2009

UDSM wagomea uteuzi wa viongozi Daruso.

WANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) wamegoma kuchagua uongozi mpya wa serikali yao, na sasa wanapinga kitendo cha mshauri wao kuteua serikali ya muda.
Uongozi wa UDSM ulitangaza kuufuta uongozi wa Serikali ya Wanafunzi (Daruso) wakati wanafunzi waliporejea chuoni hapo mapema mwaka huu baada ya mgomo wa kupinga sera ya mikopo ya elimu ya juu uliosababisha taasisi hiyo kufungwa.
Habari kutoka chuoni hapo zinaeleza kuwa wanafunzi hao walitakiwa kupiga kura kwa njia ya mtandao wa mawasiliano ya kompyuta, lakini hawakujitokeza kufanya hivyo na ndipo mshauri wa wanafunzi alipoamua kuteua viongozi wa muda.
Mshauri huyo, Dk Martha Qorro alitangaza serikali hiyo Machi 3, akitaja majina ya viongozi hao wa muda, lakini wanafunzi sasa wanapinga uteuzi huo wakisema kuwa hawakupewa haki yao ya kidemokrasia ya kuchagua viongozi wanaowataka.
“Hivi inawezekanaje uongozi wa chuo uufute uongozi wa Daruso halafu uwateue viongozi wao, tena kutoka katika uongozi walioufuta," alihoji mwanafunzi Alphonce Patrick.

"Kama walitaka wawakilishi wetu sisi wanafunzi, kwa nini wasitupe uhuru wa kuchagua viongozi tunaowataka badala ya kutuchagulia wao.“Kama chuo kimeamua kuivunja Daruso, basi kitoe nafasi kwa wanafunzi kuchagua viongozi wengine kwa hiari yao na si kuchaguliwa na ofisi ya mshauri wa wanafunzi. La sivyo huo utakuwa uongozi wa ofisi ya Dean na si Daruso.”
Lakini Mwananchi ilipowasiliana na Waziri wa Fedha, Msigwa Bahati alithibitisha kuwa wanafunzi hawakutumia haki yao walipotakiwa kupiga kura, ingawa waziri huyo wa muda alijibu kwa kifupi.

“Ndiyo mimi ni kiongozi na nimechaguliwa na ofisi ya mshauri wa wanafunzi. Kama Dean ametoa nafasi kwa wanafunzi kuchagua viongozi online na hawakuchagua, unategemea nini kifanyike? Au wewe mwandishi unatakaje," alihoji Bahati.

Ismael Emmanuel, ambaye ameteuliwa kuwa rais wa muda, aliiambia Mwananchi kwa njia ya simu kuwa ndiye kinara wa timu hiyo ya muda ya Daruso, lakini akakataa kueleza aliteuliwaje, akidai kuwa yuko darasani.
Jibu kama hilo lilitolewa na makamu wake, Patrick Damas na waziri mkuu wa serikali hiyo ya muda ya wanafunzi, Reginald Goodchance, ambaye alidai kuwa si msemaji wa Daruso hiyo.Mshauri wa wanafunzi, Dk Qorro alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa kuwa yuko mkoani Kilimanjaro.

2 comments:

  1. It's a pity i don't know swahily ... anyway I passed from here just to tell you that if Africa is part of me, Tanzania is on my heart at the top!

    ciao from
    MUZUNGU MALAIKA
    Rome Italy

    ReplyDelete