Thursday, November 3, 2011

Vurugu Arusha na Mwanza

Vurugu kubwa zimetokea jana katika majiji ya Arusha na Mwanza kiasi cha kuwalazimu polisi kutumia mabiomu ya machozi na baadhi ya watu kutiwa nguvuni.

Jana asubuhi jijini Arusha, watumishi wa daladala zinazojulikana huko kama vifodi, waliitisha mgomo kulaani kile walichokiita unyanyasaji wa polisi hatua iliyowalazimu askari hao kuingilia kati na kuwatia mbaroni zaidi ya watu 30.

Mgomo huo ulianza majira ya saa mbili asubuhi na kudumu hadi saa 5:00 asubuhi.
Pia polisi na askari wa Magereza walikuwa na kibarua kizito kuwadhibiti wafuasi wa Chadema kwenda katika Gereza la Kisongo kumwona Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema.


Polisi waliweka ulinzi mkali wakiwazuia na kuwahoji watu wote waliokuwa wakielekea njia ya Kisongo liliko Gereza hilo Kuu la Mkoa wa Arusha ambako Lema yuko mahabusu.

Wafuasi hao wa Chadema walikuwa wanataka kwenda kumwona mbunge huyo katika utaratibu wa kawaida wa kuwaona wafungwa na mahabusu katika gereza hilo siku za Jumatano, Jumamosi na Jumapili.

Baadhi ya wananchi waliofanikiwa kupenya kupitia njia za vichochoroni na kufika gerezani hapo, walikumbana na kizingiti kingine cha askari Magereza ambao waliwazuia kumwona mbunge huyo kwa madai idadi ya watu inayotakiwa kumwona ilishatimia.

Ofisa Magereza mwenye cheo cha mkaguzi msaidizi, aliyekuwa amevaa beji yenye jina la J. Mmari alizungumza na wananchi hao kwa niaba ya mkuu wa gereza hilo akisema sheria inaelekeza kuwa siku ya Jumatano wanaoruhusiwa kumtembelea mtuhumiwa ni mawakili wake na wageni wasiozidi watatu, lakini kwa busara uongozi wa gereza uliamua kuruhusu watu zaidi.

“Mpaka sasa walioingia kumwona Lema wamezidi na hatuwezi kuendelea kuruhusu kwani tangu saa 2:00 asubuhi Mheshimiwa ametembelewa na idadi kubwa na anaongea nao kwa zaidi ya dakika kila kundi. Tafadhalini wengine njooni Jumamosi na Jumapili,” alisema Mmari.

Kauli hiyo iliamsha jazba na hasira za vijana walioanza kutoa maneno makali na kumlazimu mwenyekiti wa Bavicha Wilaya ya Arumeru, Joshua Nassari kuwatuliza.

Thursday, January 13, 2011

Je, kikwete ni saafiii?

Sijui kwanini tunazungushana na kudai watu wote walioatajwa kwenye orodha ya Ufisadi wanastahili isipokuwa Rais Kikwete! Hata viongozi wanaotambua baadhi ya uzito wa tuhuma zilizotolewa na wanaodai kuwa zitiliwe maanani hujikuta wanajing'ata ng'ata kuhusu Rais Kikwete. Baadhi ya watu wamefikia mahali pa kulaumu kina Dr. Slaa kumuweka Kikwete katika kundi hilo kwani JK ni safi! Hata hivyo ushahidi wote uliopo unaonesha kuwa JK siyo safi na yeye ndiyo awe wa kwanza kujibu tuhuma zilizoelekezwa kwake!

a. Mkataba wa IPTL ulisainiwa yeye akiwa Waziri wa Nishati na Madini. Hakuna mkataba mbovu kama huo. Kushindwa kwake kutetea maslahi ya nchi akiwa Waziri na kulisababishia Taifa hasara kubwa ilikuwa ni kilele cha kutokuwajibika na kushindwa kuongoza. Akiwa Waziri mwenye dhamana ya nishati Ndg. Kikwete alitakiwa kuhakikisha kuwa serikali ya Jamhuri ya Muungano inaingia kwenye mkataba ambayo inaweza kujitoa pasipo kupata adhabu kubwa. Alishindwa na hivyo kuoneshea kutokuweza kusimamia maslahi ya nchi.

b. Wakati Rada ya bilioni 50 inanunuliwa, Ndg. Kikwete alikuwa ni Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Uhusiano wa Kimataifa na wakati sakata lenyewe linaanza alikuwa ni Waziri wa Fedha. Akiwa Waziri mwenye dhamana hiyo alishindwa kabisa kufuatilia ukweli kuwa kampuni ya BAE siyo mali ya serikali ya Uingereza na ya kuwa rada yenyewe ilikuwa imeongezwa kwa asilimia 24. Kiasi hicho kinakaribiana kabisa na wastani wa asilimia 20 za fedha za umma zinazopotea katika manunuzi ya serikali (public procurement).

Alishindwa kuhakikisha kuwa maslahi ya Taifa letu yanalindwa na alipopata nafasi ya kuonesha busara aling'aka na kusema "kwanini sisi ni idara ya Benki ya Dunia? ni kututukana kudai kuwa tusubiri Benki ya Dunia kutuamulia nini kinatufaa".

Ndio maana leo hii anapokuja na kuzungumza kuwa hawezi kuamini kuwa nchi kama Uingereza inaweza kuacha kampuni "yake" kurusha rada hiyo kwa bei hiyo wengine tunamshangaa kwani alikuwa na nafasi zaidi ya 20 ya kuweza kupinga ununuzi huo lakini alikuwa ni kinara wa kutetea tenda hiyo ya rushwa! Ni kuelewa hilo ndio utaona ni kwanini hakutaka watu wamuulize Rais Mkapa juu ya suala la rada, kwani miongoni mwa wahusika wakubwa ni yeye mwenyewe Kikwete.

c. Kama nilivyoonesha hapo juu kuwa Rais Kikwete aliwahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini. Kwa hivyo nina uhakika kabisa alikuwa anajua kabisa jinsi mikataba inavyoingiwa na alikuwa na kila sababu ya kuhakikisha kuwa mikataba inalinda maslahi ya nchi na kunufaisha nchi wakati inawapatia wawekezaji faida ya kibiashara. Kwa kitendo chake yeye mwenyewe kuwa ukaribu na wafanyabiashara hao hasa swahiba wake ambaye ni mmiliki mkubwa wa ardhi yenye vito na madini Bw. James Sinclair, Rais Kikwete tangu akiwa Waziri wa Nishati na Madini na baadaye Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje amekuwa mtu aliyetiwa upofu na "dhahabu".

Wakati Rais Mkapa na Yona wanajipatia tenda ya Kiwira, Rais Kikwete na Msabaha walikuwa wanajisogeza karibu na Kampuni ya Tanzania Royalty Exploration ambapo kuna madai kuwa Msabaha na Kikwete walikuwa na "hisa" za kiasi fulani. Kampuni hiyo ya TRE iliingia mkataba na Barrick Gold kuwa inapovumbua madini katika ardhi inayomiliki basi Barrick wanakuwa wanunuaji wa kwanza.

Ni wao TRE waliouzia Buzwagi kwa Barrick na maeneo mengine kadhaa kwa makampuni mengine. TRE inaponufaika kwa mikataba mibovu ambayo serikali inaingia na makampuni ya uchimbaji kuna watanzania wawili ambao nao wananufaika (ni wazi wapo wengine wengi na ni vigogo) na dili hizo.

Ni kwanini Barrick walikuwa wa kwanza kukubali mabadiliko ya vipengele vya mikataba yao? jibu ni ushawishi wa James Sinclair na Kikwete ili kutetea kilicho chao. Kwa yale makampuni ambayo hayana ukaribu wa James Sinclair na Kikwete (JK alimualika JS kwenye kuapishwa kwake na mara nyingi amekuwa mgeni wake akija US, na binti ya JS aliyeko Tanzania ni rafiki wa karibu) basi imekuwa vigumu kuwashawishi kubadili vipengele hivyo.

Ndio maana hadi leo hii si kweli kuwa kupitia vipengele na kuzungumza na "wakubwa" hao kuhusu mikataba kumekoma kama alivyodai mjasiriamali mwingine Nazir Karamagi alipokuwa akijaribu kupangua hoja za Zitto. Ukweli ni kwamba kamba waliitundika wenyewe serikali na ni wenyewe walioziweka shingo zao humo! wawekezaji wanatishia kuondoa kigoda!! Serikali inabembeleza!

Anapozungumzia matatizo ya mikataba Rais Kikwete anazungumzia kana kwamba tatizo ni kipengele kimoja tu! Hajachukua muda kufuatilia uzito wa hoja hizo kwani kwake ni kelele!

d. Kikwete si Safi kwani amewalinda watu wachafu! Waswahili walisema ukiwa na urafiki na wezi, usishangae watu wakakuhisi na wewe mwizi! Rais Mkapa anapomlinda mjasiriamali Mkapa, aliposhindwa kumsimamisha kazi mara moja Ditto na kuamua kumuacha ajiuzulu huku akiendelea kupata mafao yake alionesha udhaifu mkubwa wa uongozi!

Rais Kikwete amekuwa mtetezi wa wabadhirifu akikesha kutoa vitisho hewa akijaribu kutetemesha mabua na kuangusha vichuguu huku milima ikiendelea kuganda theluji! Ukimya wake kama ule wa Mkapa ni ishara wazi kuwa walifeli darasa la Mwalimu!

Anapoona kuwa madai ya ubadhirifu Benki Kuu, matumizi mabaya ya madaraka, ubadhirifu, n.k kuwa "kelele za upinzani" na kuwa "ndiyo demokrasia" anaonesha udhaifu mkubwa usiomstahili kiongozi wa nchi. Haiwezekani upotevu wa mabilioni ya fedha, matumizi mabaya ya madaraka kuwa viwe ni "kelele" tu!

Rais ni lazima we mtu ambaye hapuuzii masuala mazito na hayafanyi kuwa ni ya kijinga. Kwa mtu kuwa mpinzani hakuifanyi hoja yake kuwa "kelele". Leo hii wana CCM wenzake wanazungumza wazi kuhusu tuhuma hizi na kudai kuwa wanaotuhumiwa (akiwemo yeye mwenyewe) wajibu siyo suala la kupuuzia!

e. Rais Kikwete ameonesha na anaendelea kuonesha udhaifu mkubwa wa maamuzi hasa kwa kuwa mtu wa kusita sita na ambaye yuko tayari kutumia uwezo wake wote kutofanya lolote. Hivi hadi nini kitokee ndipo Rais Kikwete atajua kuwa mambo haya si ya kupuuzia? Wakati Lowassa ameenda kukutana na Karamagi kule London na mkataba wa Buzwagi ukasainiwa je Rais Kikwete alifahamu ujio wa Waziri wake Mkuu? Je walikutana? Kama Rais hakujulishwa kutiwa saini kwa mkataba mkubwa namna hiyo na Waziri Mkuu anakutana na Waziri mwingine pasipo ujuzi wa Rais je haoni ni ukosefu mkubwa wa kiutawala!? Lowassa alifuata nini London na kukutana na Karamagi badala ya kukutana na Rais?

Leo hii watu wakihoji mazingira ya kusainiwa mkataba huo kwanini hiyo iitwe kelele!

Tanzania imefanya kosa kubwa kumchagua Kikwete. Kosa hilo vizazi vijavyo vitasimulia kama hadithi, kuwa "hapo zamani za kale kulikuwa na mwana CCM mmoja ambaye aliwapo watu matumaini sana kabla ya uchaguzi. Watu wengi waliamini kuwa mwanaCCM huyo ndiye atakuwa mkombozi na kiongozi wa kuwaonesha njia ya kufikia nchi ile ya ahadi. Walipomchagua kwa asilimia 80 ya wapiga kura, Watanzania walijawa na matumaini... Miaka miwili baadaye watanzania walishika vichwa vyao kujuta, kwani waliyemdhania ndiye kumbe siye... !! "....

Kama Rais Kikwete hatabadili mwelekeo wa uongozi wake, na kama ataendelea kufanya kazi kana kwamba madai na hoja zinazojengwa ni "kelele" tu na hivyo kuendelea kufumba macho ufisadi unaoendelea nchini (na hapa simaanishi rushwa ya kutoa na kupokea tu, namaanisha matumizi mabaya ya madaraka, n.k).

Thursday, December 23, 2010

Wednesday, December 15, 2010

UN kusaidia TZ dola 773 milioni za Marekani

Serikali ya Tanzania na Umoja wa Mataifa (UN) ,wamesaini makubaliano ya utaratibu mpya wa misaada unaojulikana kama UNDAP utakaodumu kwa miaka 4 kuanzia mwaka ujao wenye thamani ya dola 773 milioni za Marekani.

Makubaliano hayo yalifanyika jana, jijini Dar es Salaam ,baina ya serikali ya Tanzania na Umoja wa Mataifa , ukiwa na lengo la kuondoa umasikini nchini kwa kusaidia Mfuko wa MKUKUTA na MKUZA.


Hii ni mara ya kwanza serikali ya Tanzania na UN kufikia hatua ya kusaini makubaliano hayo ikiwa ni sawa na mkataba kati ya nchi ya Tanzania na UN kwa miaka minne.

Tukio hilo lilishuhudiwa na msaidizi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Ramadhani Khijjah na Alberic Kacou, kutoka UN jijini Dar es salaam.

Khijja alisema kuwa serikali ya Tanzania iko tayari kufanya kazi na UN na kweli ni kwamba kuna UN tu na si nyingine .

Alisema Tanzania haikuwa nyuma bali inajitahidi kupiga hatua kibiashara na huu mkataba unaonyesha ni namna gani Tanzania ilivyodhamiria kupiga hatua kimaendeleo.

Akizungumza kwa niaba ya wawakilishi wa Umoja wa Mataifa ,Balozi wa Ireland, Lorcan Fullam, alitoa pongezi kwa muungano huo wa serikali ya Tanzania na Umoja wa Mataifa akifafanua kwamba kinachoangaliwa zaidi ni nini kitafanyika kwa hiyo miaka minne ijayo kwa sababu sio mbali.

Wednesday, December 1, 2010

Baraza la JK la kulipa fadhila-Prof Shivji.

Mhadhiri maarufu wa masuala ya kisiasa na kijamii, Prof Issa Shivji ameliponda baraza jipya la mawaziri akisema kuwa limeundwa kwa utashi wa kisiasa ili kulipana fadhila.

Prof Shivji, ambaye ni mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, pia aliungana na wadau wengine wanaolilia mabadiliko ya katiba akisema suluhisho la matatizo mengi nchini ni kuundwa na katiba mpya itakayotokana na utashi wa wananchi.

Maoni yake yametokana na uteuzi wa baraza lenye mawaziri 50 uliofanywa na Rais Jakaya Kikwete ambaye aliongeza mawaziri wapya 24 na kutema tisa baada ya kuchaguliwa kuongoza nchi kwa miaka mitano ya mwisho ya serikali ya awamu ya nne.

Baraza hilo lilianza kazi zake rasmi jana, lakini katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Channel Ten Shivji, ambaye amebobea kwenye sheria lakini ambaye amejishughulisha sana na siasa, alilizungumzia baraza hilo kuwa ni limeundwa kwa lengo la kulipa fadhila na si kwa kuzingatia uwezo.


“Kimsingi na kimantiki uteuzi na ukubwa wa baraza la mawaziri kwa nchi nyingi za Kiafrika na hata hili la Tanzania unatokana na utashi wa kisiasa hasa undugu na urafiki kwa lengo la kulipa fadhila," alisema Profesa Shivji.

"Mara chache uteuzi huzingatia mahitaji ya wananchi na maslahi ya taifa kwa ujumla. Ukubwa wa baraza si kipimo cha utendaji bora.’’


Profesa Shivji, ambaye alikuwa mhadhiri wa UDSM, alifafanua kwamba ndio maana wagombea ubunge walilazimika kumpigia debe mgombea urais wakati wa kampeni kwa lengo la kutaka kulipwa fadhila ya kuteuliwa kuwa waziri au naibu waziri

Alisema suala hilo pia linachochewa na sheria inayokazi9misha waziri ateuliwe kutoka miongoni mwa wabunge.

Profesa huyo alisema kimsingi kazi ya mawaziri ni kusimamia sera pamoja na utendaji na si vinginevyo.

Kikwete, ambaye aliunda baraza la mawaziri 60 alipoingia Ikulu kwa mara ya kwanza mwaka 2006, aliteua mawaziri watatu zaidi ya wale waliokuwemo kwenye baraza lililomaliza muda wake ambalo aliliteua mwaka 2008 baada ya Edward Lowassa kujiuzulu uwaziri mkuu.

Baraza hilo pia linaponekana kuzingatia uwakilishi wa kanda na mikoa na linajumuisha mabadiliko kadhaa ambayo mkuu huyo wa nchi aliyaelezea kuwa yamefanywa ili kuongeza ufanisi, ikiwa ni pamoja na kuhamisha baadhi ya idara kutoka wizara moja hadi nyingine na kuigawa Wizara ya Miundombinu kuwa katika wizara mbili.


Prof Shivji alisema kufanya mabadiliko ya muundo wa Baraza la Mawaziri bila kubadilisha mfumo ni sawa na kufanya bure.

Lakini alimshauri Rais Kikwete kuwa makini katika uteuzi wa makatibu wakuu wa wizara pamoja na manaibu wao, akimtaka azingatie uwezo katika utendaji.

“Katibu mkuu ndiye mtendaji wa shughuli za kila siku za wizara. Kazi ya waziri ni kusimamia sera na utendaji tu," alisema Prof Shivji.

“Rais Kikwete anatakiwa kufanya kazi ya ziada katika kuteua makatibu wakuu... muhimu ni lazima wawe wasomi wazuri, wenye uwezo na watakaokuwa wepesi wa kuelewa wanachoshauriwa na wataalamu,’’ alisema Profesa Shivji


Profesa huyo alisema kulingana na hali ya uchumi ilivyo nchini, serikali ya Kikwete inakabiliwa na changamoto nyingi hasa ya kuhakikisha nchi inazalisha zaidi kuliko ilivyo sasa.

Alisema pamoja na kwamba asilimia 80 ya Watanzania ni wakulima, sekta hiyo inachangia katika pato la taifa kwa asilimia 26, akifafanua kuwa kiwango hicho kinamaanisha kuwa Watanzania wanazalisha kwa asilimia 26.


Mhadhiri huyo ambaye ni mwanaharakati wa ardhi alisema katika miaka ya 50, kilimo nchini kilifanya vizuri na nchi ilikuwa ikizalisha kwa wastani wa zaidi ya asilimia 50, lakini kiwango hicho kimekuwa kikishuka kila mwaka.

“Ukiniuliza sababu ya hili, nitakueleza tu kuwa tumeua kwa makusudi viwanda vyetu pamoja na kilimo,’’ alisema


Alifafanua kwamba ili nchi yoyote iweze kuendelea, ni lazima uzalishaji wake uwe mkubwa na hasa kutoka kwa wazalishaji wadogo wa vijijini na kwamba uchumi unayumba kutokana na wazalishaji wadogo kutothaminiwa.

Alisema ili nchi ipige hatua ya kimaendeleo ni lazima kilimo cha umwagiliaji kipewe nafasi kubwa pamoja na kuwepo kwa zana za kisasa za kilimo, ikiwa ni pamoja na wakulima kukopeshwa fedha kutoka katika benki.

“Wanasema Tanzania ni maskini lakini cha ajabu ina benki nyingi tena za kimataifa ambazo haziko tayari kuwakopesha wakulima,’’ alisema.

“Serikali ndio ilipaswa kuwa dhamana kwa wakulima kukopa lakini haiko tayari katika hilo.’’


Gwiji huyo wa sheria na aliyebobea katika masuala ya katiba alikwenda mbali na kusema pamoja na mambo mengine suluhisho la matatizo mengi nchini ni kuundwa kwa katiba mpya itakayotokana na utashi wa wananchi.

Profesa Shivji alisema kinachopaswa kuzingatiwa kwa sasa ni ni jinsi katiba hiyo itakavyoundwa ili iweze kupata uhalali wa wananchi wote.

“Hapa napenda wananchi waelewe kuwa unapozungumzia katiba mpya, huzungumzii muundo wake bali jinsi inavyotungwa ili iweze kupata uhalali wa wananachi wote na si tu yale yatakayokuwemo ndani yake,’’ alisema


Alifafanua kwamba katiba ya sasa ambayo ni ya mwaka 1977, ilitokana na mfumo wa kisiasa wa chama kimoja pamoja na hivyo kushirikisha watu wachache.

Alisema hali hiyo inaifanya katiba iwe haikidhi utashi wa Watanzania walio wengi kutokana na kwamba haiendani na mazingira ya kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni yalivyo sasa.

Alitoa mfano wa katiba mpya ya nchini Kenya ambako alisema ilitokana na wananchi na kwamba pamoja na mambo mengine imepunguza madaraka ya rais, ikiwa ni pamoja na ukubwa wa Baraza la Mawaziri kutokana na kueleza bayana kuwa lisiwe na chini ya watu 14 na lisizidi watu 24.


“Wamekwenda mbali zaidi na sheria kutaka wanaoteuliwa kuwa mawaziri wasiwe wabunge, bali wathibitishwe na Bunge,’’ alisema .

Lakini Waziri wa Sheria na Katiba, Celina Kombani alikaririwa jana akisema kuwa serikali haijawa tayari kuunda katiba mpya na kwamba itaendelea na mtindo wa kufanya marekebisho ya sheria hiyo wakati wowote itapolazimika.

Wednesday, November 24, 2010

familia ya Lowassa yachunguzwa uingereza-baada ya kuhamisha 1bil kutoka Tanzania.

Mtoto wa aliyekuwa Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa anayeitwa Frederick Lowassa anachunguzwa na Kitengo Maalumu cha Polisi wa Kimataifa wa Uingereza wanaofuatilia utata wa uhamishaji fedha kutoka Tanzania.

Fedha hizo zinahusishwa na ununuzi wa nyumba yenye thamani ya pauni za Uingereza 475,000 (takriban Shilingi bilioni moja) katikati ya Jiji la London, .

Hata hivyo, watu walio karibu na Frederick wameelezea kwamba kijana huyo hakuwahi kununua nyumba; bali aliwahi kutaka kupanga kwa ajili ya kuishi akiwa masomoni nchini Uingereza na fedha nyingine alizituma kwa ndugu yake aishie nchini humo.

Nyumba ambayo inatajwa katika maelezo ya awali iko mtaa wa Leinster Gardens, jijini London.

Hata hivyo, hakuna ofisa yeyote wa Serikali ya Tanzania aliyekuwa tayari kuzungumzia suala hilo, pamoja na kuwapo taarifa kwamba tayari vyombo vya dola vya Tanzania vimekwisha kuhusishwa katika uchunguzi huo.

Maofisa wa Polisi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (CID) wanaohusika na uchunguzi wa fedha haramu, wamekwepa kuzungumzia suala hilo na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Robert Manumba, hakuweza kupatikana, na alielezwa kuwa nje ya nchi kikazi.

Ofisa wa CID aliyeelezwa kuongoza kitengo kinachochunguza makosa ya uhalifu wa fedha na nyaraka, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Samson Kasala, alikanusha kufahamu chochote kuhusiana na suala hilo.


Taarifa zinaeleza kwamba Kitengo cha Ufuatiliaji wa Fedha Haramu (Financial Intelligence Unit-FIU) kilichopo chini ya Wizara ya Fedha nchini, kilipokea taarifa kutoka Polisi wa Kimataifa wa London, Uingereza, wakitaka taarifa muhimu kuhusiana na Frederick, kabla ya kitengo hicho kuomba msaada wa polisi.

Hata hivyo, Kamishna wa FIU, Herman Kessy, hakuweza kupatikana wiki iliyopita akielezwa kuwapo nchini Afrika Kusini kikazi, lakini hata aliporejea wiki hii hakuweza kutoa ushirikiano.

FIU imeanzishwa chini ya Sheria ya Udhibiti wa Fedha Haramu ya mwaka 2006 (Anti-Money Laundering Act-2006) kwa kuundiwa kanuni mwaka 2007, lakini hadi sasa kitengo hicho kimekuwa kikiendeshwa na maofisa watano tu, Kamishna Kessy, mchambuzi mmoja, mtaalamu wa mawasiliano na wasaidizi wawili wasio wataalamu, kitengo kilichopaswa kuendeshwa na watu wengi zaidi kutokana na unyeti wake.

Habari zinaeleza kwamba hata ofisa wa Polisi aliyewahi kuhamishiwa FIU kwa kazi maalumu alijikuta akitengwa na kutopangiwa kazi na maofisa hao ambao wengi wanatoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), baada ya kuwa wameaminiwa sana na uongozi wa juu wa serikali.

Kwa mujibu wa taarifa hizo ambazo bado zinafanyiwa kazi, Frederick ambaye baba yake alijiuzulu Uwaziri Mkuu kwa kuhusishwa na kashfa ya ununuzi wa mitambo ya kuzalisha umeme iliyokabidhiwa kwa kampuni tata ya Richmond Development LLC, anadaiwa kufanya mawasiliano kupitia kampuni ya uwakala iliyotajwa kwa jina la ‘Mishcon’.

Nyaraka alizowasilisha, zilidai kuwapo ubia kati ya mtuhumiwa huyo na kampuni tatu ikiwamo Integrated Property Investment(T) Ltd na Barare Ltd Company.

Mkataba huo unaonyesha kuwa Frederick Lowassa ana hisa kwenye kampuni hizo, na kwamba fedha za ununuzi wa nyumba hizo zinatokana na fedha za malipo ya hisa anazopata kutokana na kampuni hizo.

Hata hivyo, mkataba huo unaonyesha kusainiwa Machi 25 mwaka 2009 siku moja baada ya Frederick Lowassa kusaini mkataba kati yake na kampuni ya Mishcon kama wakala wake katika ununuzi wa jengo hilo.

Pia aliwasilisha nyaraka zinazoihusisha kampuni ya Alphatel kama moja ya kampuni ambayo pia yeye ni mkurugenzi wake ambayo pia ni chanzo chake kingine cha fedha anazotumia kununua jengo hilo.

Taarifa zimedokeza kuwa ununuzi huo ulikwama baada ya kushindwa kutoa malipo hayo kwa mujibu wa mkataba kati yake na wakala wa ununuzi wa nyumba hiyo (kampuni ya Mishcon) ambao ulimtaka awe amekamilisha kulipa fedha hizo kabla ya Aprili 14, mwaka 2009.

Hata hivyo, siku chache baadaye ndani ya mwezi huo wa Aprili, Frederick aliipelekea Mishcon kiasi cha pauni za Uingereza 199,940 zikitokea kwenye kampuni ya ununuzi fedha ya Wall Street Exchange.

Aidha kiasi cha pauni 100,000 kiliingizwa kwenye akaunti ya kampuni hiyo hiyo ya Mishcon kwa fedha taslimu katika mikupuo 12 tofauti zikitokea kwenye matawi tofauti ya benki ya NatWest Bank plc iliyoko Kaskazini mwa Jiji la London.

Mazingira ya kuingizwa fedha hizo kwenye akaunti ya wakala huyo ( Mishcon) ndiyo yameifanya Taasisi ya SCD 6 Economics and Specialist Proceeds of Corruption Unit ya Uingereza inayosimamia uchunguzi wa sakata hilo kuwa na mashaka makubwa kuhusu uhalali wa fedha hizo.

Kutokana na mazingira hayo, SCD 6 Economic and Specialist Crime Proceeds of Corruption Unit yenye ofisi zake Victoria Block, New Scotland Yard, London, ililazimika kuwasiliana na FIU ikitaka maelezo ya awali kuwezesha kufanyika kwa uchunguzi kuhusu fedha hizo.

Hata hivyo,Fredrick alikana kununua nyumba Uingereza lakini alikiri kuwahi kutuma fedha huko.


Hata hivyo , maelezo ya awali ambayo yalitakiwa kutoka Tanzania na makachero hao wa Uingereza, ni pamoja na kutaka kufahamu kama kweli Frederick Edward Lowassa amezaliwa Agosti 26, 1977, Mwanza Tanzania na anamiliki hati ya kusafiria yenye namba AB 109402 iliyotolewa Tanzania na kwamba anwani yake nchini Uingereza ni 71 Hendrix Drive, Milton Keynes, MK8 0DY.

Pia makachero hao waliitaka Serikali ya Tanzania kutoa ufafanuzi wakitaka kujua kama Frederick Lowassa ni mbia katika kampuni za Alphatel Partnership (Tanzania) Barare Ltd na Intergrated Tanzania Limited, kampuni ambazo zimefahamika kumilikiwa na familia ya Lowassa.

Asasi hiyo ya Uingereza pia imeomba kujua kama FIU wana taarifa zozote za uhalifu dhidi ya Frederick Lowassa na kama baba yake Edward Lowassa anachunguzwa kwa tuhuma yoyote ya rushwa na mamlaka za uchunguzi wa rushwa nchini Tanzania kuhusu fedha haramu.

Uchunguzi wa awali uliofanywa na vyombo vya dola, ulielezwa na taarifa hizo kwamba Frederick Lowassa si mbia katika kampuni hizo na kwamba Barare Ltd wenye hisa ni Edward Ngoyai Lowassa mwenye hisa 500 na Regina Mumba Lowassa mwenye hisa 500 huku wakurugenzi wakiwa ni hao hao.

Ofisa wa Uingereza anayesimamia uchunguzi huo, George Simpson, amedai kwamba kanuni za uchunguzi kuhusiana na kesi zenye mguso wa kisiasa huwazuia kukanusha au kuthibitisha kuhusu uchunguzi unaoendelea hadi pale wanapofikia hatua ya kukamata mtuhumiwa ama anapofikishwa mahakamani.