Spika wa Bunge, Anne Makinda jana aliizima hoja ya Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee kuhusu umiliki wa mashamba makubwa yasiyoendelezwa wakati wa kujadili hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambayo ilihitimishwa bungeni jana.
Mdee alivutana na Spika Makinda wakati wa kujadili bajeti hiyo kifungu kwa kifungu, Mdee alitaka kufahamu kauli ya Serikali kuhusu kampuni zinazomiliki ardhi bila kuziendeleza na hatua zinazochukua kuhakikisha zinarudishwa kwa wananchi.
Baada ya kuuliza swali hilo huku akisisitiza kutoa shilingi, Spika Makinda alimtaka kukaa chini kwa kuwa hoja yake haina mashiko ya kufanya hivyo.
“Kaa chini, nakwambia kaa chini,” alisema Makinda huku Mdee akionekana kuendelea kuzungumza... “Nasema kaa chini,” alirudia na Mdee kukaa huku akikipeperusha karatasi hewani kuonyesha kutokubaliana naye.
Awali, Mdee alisema shamba la Simanjiro ambalo Halmashauri ya wilaya hiyo ilipendekeza mwekezaji kupewa ekari 500 lakini Wizara ya Ardhi iliidhinisha ekari 25,000 ambazo mwekezaji hajaziendeleza zote wakati mashamba ya Kisarawe na mashamba ya mkonge Tanga ambayo wawekezaji wameyakopea fedha nayo hadi sasa hayajaendelezwa.
Alitaka kauli ya Serikali kuhusiana na hali hiyo na jinsi ya kurudisha mashamba hayo katika miliki ya umma. Mbunge mwingine aliyetishia kutoa shilingi ni Dk Faustine Ndungulile wa Kigamboni (CCM), akijikita katika suala la ujenzi wa mji mpya wa Kigamboni akisema wananchi wake hawakushirikishwa katika mipango ya ujenzi huo.
No comments:
Post a Comment