Monday, June 3, 2013

CHADEMA yaitaka serikali kuacha kuibambikia kesi

Dk. Willibrod Slaa,Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),amemtaka Rais Jakaya Kikwete na chama chake waache kuwabambikizia kesi za ugaidi na uchochezi wapinzani.


Dk. Slaa alisema hata kama viongozi na wanachama wa CHADEMA wataendelea kubambikiwa kesi hawatoacha kupambana na CCM hadi chama hicho kitakapoondoka madarakani.

Kauli hiyo aliitoa juzi katika viwanja vya Uwanja wa Ndege mjini Morogoro alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara ambapo alisema wanaamini Rais Kikwete ameshindwa kuisimamia serikali yake.

Alisema kushindwa huko kwa Rais ndiko kunakomfanya kila kukicha kutafuta makosa ya kuwabambikia wapinzani wanaoupinga utawala wake mbovu.

“Tutaendelea kupambana na serikali ya Kikwete kwa njia yoyote hadi itakapoondoka,nyie tubambikezieni kesi za ugaidi, uchochezi na nyingine za kusingiziwa lakini hatutakubali watoto wa baadaye wachezewe kwenye mambo nyeti kama elimu,” alisema.

Alisema serikali ya CCM imeshindwa kusimamia uongozi bora tangu miaka ya 1990 kwa kuondoa misingi ya utawala na kuingiza misingi mibovu inayolita hasara taifa na wananchi wake kwa kujineemesha watawala peke yao.

Alibainisha kuwa watawala sasa  hivi wanaichezea nchi kwa kutoa vituko vya kila aina ikiwemo cha hivi karibuni ambapo serikali ilifuta matokeo ya kidato cha nne 2012 na kuyapitia upya.

Aliongeza kuwa pamoja na kuyapitia upya bado idadi kubwa ya wanafunzi wamefeli mitihani hivyo CHADEMA haitokubali CCM iendelee kuharibu taifa na kizazi kijacho.

Alisema hawezi kufanya unafiki wa kwenda kwenye majumba ya ibada kuomba amani kama wafanyavyo viongozi wengine kwa shinikizo la Rais Jakaya Kikwete wakati Watanzania wanataabika kwa utawala mbovu.

Alibainisha kuwa Watanzania wanakabiliwa na matatizo mengi yakiwemo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa ambayo ni chanzo cha kutoweka kwa amani.

Alisema Kikwete na serikali yake bado hawajayaelewa au wanayapuuzia matatizo yanayochangia kuvurugika kwa amani.

Dk. Slaa alitoa mfano wa migogoro ya ardhi inayoikumba mkoa wa Morogoro kila mara inasababishwa na ufinyu wa uadilifu kwa watumishi wa serikali ambao ni matunda ya serikali ya CCM.

“Amani haihubiriwi ikaja au ikaimarika, hujengwa na kuimarishwa kwa misingi bora na uadilifu katika uongozi wa nchi ambao sasa haupo,” alisema.

“Sitaki unafiki wa kwenda eti kuombea amani, amani ipi? leo kuna taarifa za kila aina juu ya uovu ikiwemo wizi wa rasilimali za nchi, wananchi wakiendelea kutaabika na ugumu wa maisha kila kukicha lakini serikali imekaa kimya.”

Awali kabla ya Dk. Slaa kuhutubia Mwenyekiti wa Baraza la Vijana CHADEMA (BAVICHA) John Heche aliwataka wananchi wabadilike kwa kuiondoa CCM madarakani ili wapate maisha bora.

Alisema watawala wanajifanyia watavyo kwa kujichukulia rasilimali zilizomo nchini kwa manufaa yao kwa sababu ya kujiamini wataendelea kutawala milele.

“Nchi hii ili iendelee inahitaji utawala ubadilike na wa kuubadili ni ninyi wananchi...’ipigeni’ chini CCM 2014 na 2015 na kutuweka sisi tukishindwa kutekeleza tuliyokubaliana na ‘tupigeni’ chini wekeni chama kingine chochote,” alisema.

No comments:

Post a Comment