Tuesday, May 28, 2013

Hatimaye Lipumba akiri kumbeba JK mwaka 2010

     Hatimaye mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amekiri kukihusisha chama chake cha CUF na “kumnusuru” Rais Jakaya Kikwete katika uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka 2010.



Profesa Lipumba alitoboa siri hiyo katika Msikiti wa Idrissa, Kariakoo, jijini Dar es Salaam, alikokwenda kuswali swala ya Ijumaa katika mojawapo ya Ijumaa za mwezi huu.


Kwa mujibu wa video ya tukio hilo iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii mapema wiki hii, Profesa Lipumba alikaribishwa kuzungumza na waumini hao mara baada ya utangulizi uliotolewa na Imamu wa msikiti huo, Sheikh Ali Basaleh, aliyemtaka awaeleze Waislamu hali ya kisiasa nchini kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2015.


Huku akisisitiza juu ya umuhimu wa mshikamano wa kiimani, Profesa Lipumba alianza kwa kuzungumzia matokeo ya uchaguzi mkuu wa 2010, na ushindani mkali wa kisiasa uliokuwapo.

Alisema hawaoni matunda ya jitihada walizofanya kumnusuru Rais Kikwete asishindwe kwa mantiki ya udini (uislamu), kwani hata chini ya uongozi wake, Waislamu wameendelea kutothaminiwa.

“Ninyi masheikh mnajua vizuri zaidi hali ya kisiasa ilivyokuwa, kwamba ilibidi zifanyike juhudi za makusudi ili kuokoa jahazi. Lakini pamoja na kuliokoa jahazi, hali halisi inaonyesha mpaka sasa hakuna matunda yoyote yaliyopatikana, na tupo katika mtihani mgumu zaidi,” alisema.

Katika hali ambayo inasemekana ushindi wa Rais Kikwete ulipatikana kwa mbinu, huku wengine wakiituhumu Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa ilimnusuru mgombea wa CCM, kauli hii ya Profesa Lipumba inadokeza kwamba anajua mkakati zaidi wa kazi ya Tume ya Uchaguzi.

Katika hali isiyo ya kawaida, Profesa Lipumba anaonekana kuhamasisha Waislamu kujipanga akisema “wenzetu wameanza kujipanga” kuelekea 2015.

“Kwahiyo kama Waislamu tunataka kupata haki zetu, kama tunataka kuishi kama raia wa daraja la kwanza katika nchi yetu, lazima tujipange kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015; na sisi tuanze kujipanga kwa sababu wenzetu wameanza kujipanga, vinginevyo tutaendelea kubaki maskini na raia wa daraja la nne katika nchi yetu wenyewe.

“Mwaka 2010 wakati mshindi wa uchaguzi wa rais alipotangazwa, mimi nilikwenda kwenye hafla ya kutangazwa matokeo, na nilikwenda makusudi tu, siyo kwamba uchaguzi ulikuwa huru na wa haki, ila nilikwenda makusudi kwa kujua hali ya kisiasa ilivyokuwa wakati huo.

“Huku nilikutana na Sheikh Basaleh. Nilipokutana naye, alinipongeza; sijui kama yeye anakumbuka, akaniambia ‘umeweka mbele imani yako na umekuwa mwelewa wa mambo.’”

Hata hivyo, licha ya Profesa Lipumba kuwaambia Waislamu wajipange kwa ajili ya uchaguzi mkuu, hakusema wajipange kupitia chama kipi.

Itakumbukwa kuwa kumekuwepo tuhuma dhidi ya Rais Kikwete na CCM kuwa mwaka 2010 waliendesha propaganda chafu za udini zenye lengo la kuwagawa Watanzania hususan Wakristo na Waislamu kwa manufaa yao ya kisiasa.





No comments:

Post a Comment