Tuesday, May 28, 2013

Serikali yaendelea kumbeba Jairo

Utamaduni na desturi ya  serikali ya awamu ya nne wa kutotekeleza maazimio ya Bunge kwa kuwachukulia hatua watendaji wake waliotiwa hatiani na kamati teule, huenda ukamnufaisha aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo.


Hatua hiyo ni kutokana na msimamo wa waziri wa wizara hiyo, Profesa Sospeter Muhongo, kuonyesha hayuko tayari kuchukua hatua zozote kwa Jairo aliyesimamishwa kazi kutokana na matumizi mabaya ya madaraka.

Jairo alituhumiwa kukusanya na kutumia fedha za serikali kinyume cha sheria, kanuni na taratibu za fedha za umma na kuruhusu matumizi mabaya ya fedha za umma.

Kamati teule ya Bunge iliyoundwa kuchunguza tuhuma hizo kwa kipindi cha mwaka 2011/2012, ilipendekeza serikali ichukue hatua za kinidhamu kwa Jairo.

Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni kwa Wizara ya Nishati na Madini, John Mnyika, wakati wa kuwasilisha maoni yao kwa mwaka wa fedha 2013/2014 aliitaka serikali ieleze kwa nini haikutekeleza maazimio ya Bunge.

Hata hivyo, katika kuhitimisha hoja za wabunge mwishoni mwa wiki, Waziri Muhongo aliligeuza sakata kuwa la kisiasa huku akiwashambulia CHADEMA kuwa wanafanya porojo.

“Muda wa porojo umekwisha na ndio maana mimi ukinitajia mlolongo wa kesi ukitaka nikafukue mafaili pale ofisini, mimi ni mbunge wa kuteuliwa nikapewa uwaziri nadhani hawakunituma pale kupekua mafaili,” alisema.

Muhongo alisema kwa vile CHADEMA wana ushahidi na vyombo vya dola vipo wapeleke suala hilo mahakamani.

Majibu ya waziri Muhongo yalipingwa na Mnyika wakati Bunge likiwa limekaa kama kamati kupitia kifungu kwa kifungu na kutaka apatiwe ufafanuzi wa kujitosheleza huku akitoa kusudio la kutoa shilingi kwenye mshahara wa waziri endapo asingeridhika.

Hata hivyo, kusudio la Mnyika lilitupiliwa mbali na Spika wa Bunge, Anna Makinda, ambaye alitoa muda mwingi kwa wabunge kuhoji vifungu na kisha akatumia kanuni kupisha mafungu kwa ujumla.

Akizungumzia kauli ya Muhongo, Mnyika alisema kuwa waziri huyo ni muongo na ushahidi wa kumbukumbu rasmi za Bunge (hansard) ya Julai 28 mwaka 2012 unaonyesha.

“Nilihoji kuhusu utekelezaji wa maazimio ya Bunge juu ya gesi asilia na sakata la Jairo, waziri akajibu: ‘Hafanyi kazi kwa redio na magazeti.’ Hii ni dharau kwa Bunge.

“Mwaka huu 2013 katika hotuba yangu nimehoji tena kuhusu maazimio ya Bunge ya Richmond, Kiwira, Jairo, Mpango wa Dharura wa Umeme, mafuta na gesi asilia lakini hatua hiyo ameiita porojo,” alisema.

Mnyika alisema kuwa waziri anasahau kwamba kama maazimio hayo yangetekelezwa kwa wakati nchi isingekuwa na mgogoro katika gesi asilia ikiwemo ujenzi wa bomba na pia uchumi usingeathirika kutokana na matatizo ya umeme.

No comments:

Post a Comment