Tuesday, May 28, 2013

CCM Tabora wazomewa

Baadhi ya viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Tabora juzi walipata wakati mgumu baada ya kuzomewa na wananchi kwenye mkutano wa hadhara.


Tukio hilo lilitokea kwenye mkutano wa hadhara ulifanyika viwanja vya stendi ya mabasi zamani ambako walihudhuria viongozi mbalimbai akiwemo mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Aden Rage.

CCM ilifanya mkutano huo baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kikiongozwa na Naibu Katibu mkuu wake, Zitto Kabwe, kufanya mkutano katika eneo hilo na kuwachongea wabunge wa CCM Tabora kuwa hawatetei wapigakura wao.

Dalili za zomeazomea zilianza mapema kwani baadhi ya wananchi walianza kuibua vicheko na kejeli kwa viongozi wa CCM huku wengine wakisikika wakisema hawataki majigambo, matusi bali barabara za lami

kutoka Tabora-Nzega, Tabora-Urambo na ile ya Itigi-Tabora na wengine wakisema 'Peoples Power'.

Wakati Katibu wa CCM Mkoa wa Tabora, Idd Ame, akizungumza kwenye mkutano huo, wananchi wachache waliokusanyika walianza kuzomea kila kiongozi huyo alipokuwa akijaribu kuikejeli CHADEMA.

“Ndugu zangu wananchi hebu angalieni mnavyodanganywa, hivi hawa CHADEMA wanajigamba kujenga barabara wakati wao siyo watoaji wa fedha…fedha zinatolewa na serikali ya CCM, hao CHADEMA ni wanafiki na waongo,” alisema Ame.

Alisema inashangaza kuona mtu anaacha jimbo lake Kigoma kwenda Tabora kuwafundisha siasa na kudai kuwa huo upumbavu.

Baada ya kauli hiyo, wananchi walipoanza kuzomea kwa nguvu na kudai wanataka sera na si matusi.

“Hapa tuko kamili endeleeni kuzomea tu…tutaumizana kwelikweli hapa msifikiri hatuwezi na tutawashitaki viongozi wa CHADEMA Tabora kwa kutufanyia fujo kwenye mkutano wetu,” alisikika akisema Katibu huyo wa CCM.

Wakati katibu huyo akitamka hayo, Mjumbe wa NEC John Mchele alikwenda jukwaani na kumnong`oneza katibu huyo, ndipo ilizuka fujo kubwa huku Green Guard wa CCM wakitembeza mkong`oto kwa baadhi ya wananchi waliokuwa wakionesha ishara ya vema.

Tafrani hiyo ilidumu kwa dakika 20 na ndipo askari polisi walipoongezwa na mkutano kuendelea.

No comments:

Post a Comment