Monday, April 6, 2009

Tanzania:tatizo letu ni nini hasa?

Je, tatizo ni Elimu? (kwamba wananchi wengi hawana, na vyombo vya habari pia vimo kwenye mkondo huo huo, mambo ya Mzumbe kwa mfano ya vyeti feki), Uzalendo?(viongozi na sisi sote), Rushwa? Uvivu wa Kufikiri? (Che Nkapa aliwahi kudai hivyo)au Siasa mbovu? Kutoheshimu Taaluma (ushauri wa kitaalam kutoka kwa wasomi na hasa wazalendo)? Je, mkazo tuweke wapi ili tujikwamue?

Kwa ufupi ni kuwa Tatizo siyo sera (kwani tunazo nzuri), siyo elimu (kwani tuna maprofesa hadi wenye shahada feki), siyo uvivu (kwani hilo ni tusi kwa Watanzania) na wala siyo dira (kwani dira tunazo hadi za mwaka 2020!). Tatizo tulilonalo sisi ni la kiongozi.

Tanzania tuna viongozi wababaishaji wasio na uwezo wa kutekeleza maamuzi ya kiserikali au chama. Viongozi wengi hawajui kuongoza, ingawa wengi wanajifanya wanajua kutawala! Ni viongozi ambao hawajui kuthubutu au kuchukua maamuzi ambayo yatawaharibia sifa au umaarufu wao! Ni viongozi ambao hawapendi kumuudhi mtu au kumkasirisha mtu. Ushahidi wa hili ni habari za hivi karibuni kuwa WM amekataa ripoti ya maendeleo ya wilaya fulani huko Kigoma, kitu kilichosababisha viongozi wa wilaya za Iringa (atakakotembelea hivi karibuni kuanza kujihami. Kwa vile hawajui kuongoza, viongozi hawa uchwara wanajaribu kwa kila mbinu kujifanya wanajua kutawala!

Ni kwa sababu hiyo basi, utakuta viongozi wanaishia kukaa maofisini, kuweka majalada sahihi, kuangalia taarifa wazisoweza kuzielewa n.k! Ni viongozi hao ambao wanasubiri aliyejuu yao kuwaonesha njia (kama alivyofanya WM) na ambao hawatendi kwa kufuata maamuzi yanayoeleweka. Ni kwa sababu hiyo utakuta basi, jambo ambalo inabidi lifanywe na Mkuu wa Wilaya linapelekwa kwa mkuu wa Mkoa ambaye naye kwa ufinyu na udhaifu wa uwezo wake wa uongozi atapiga simu ofisi ya Tawala za Mikoa kuomba maelekezo!!

Ni viongozi hao ambao katika akili zao zilizodumaa kiuongozi wanaangalia suala fulani linamhusu mtu gani. Kwa viongozi hao, kuna haki ya watu mashuhuri na haki ya watu wa chini. Wanapokabiliana na tatizo wakiwa na mwenendo huo wa mawazo, utajikuta wanapinda sheria na wakati mwingine kuivunja kabisa! Migogoro ya ardhi kwa mfano, isingetokea kama haki ya watu wa chini ingekuwa inaonekana ni haki sawa na ile ya watu mashuhuri!! Viongozi wetu hawajui hilo.

Akitokea bwana Rweyemamu ambaye ni mfanyabiashara mashuhuri na akataka kujenga kwenye eneo fulani pale Ilemela Mwanza, eneo ambalo linamilikiwa na mkulima Mzee Masanja kwa uhalali wake, basi kiongozi wetu atatumia uwezo wake wa kiutawala kuhakikisha kuwa Bw. Rweyemamu anapata eneo hilo!!! Bw.Masanja ataenda Polisi na Mahakamani kulalamikia jambo hilo. Akifika huko tatizo ni lile lile. Bi. Hakimu anaangalia hiyo kesi na kukuta kuwa inamhusu Bw. Rweyemamu ambaye ni mtu maarufu!! Kwa sababu anazozielewa yeye anatupilia mbali kesi ya Masanja. Miaka inaenda na kurudi hadi anapotokea kiongozi ambaye hajali sura za watu au hadhi zao! Kiongozi huyo anasema kwa halali eneo ni la Masanja!! Anamnyang'anya Rweyemamu kiwanja na kukirudisha kwa Masanja. Watu wanamuona mtu huyo mkombozi!!! Mfano huo unaweza kutumiwa mahospitalini, mashuleni, kwenye mikopo ya mabenki n.k!

Kiongozi wa ngazi ya chini anayeonekana kufanya kazi vizuri haachwi huko. Kama ni hakimu mzuri, utasikia anapandishwa cheo na kuwa Jaji wa Mahakama ya juu, kama ni mwalimu atapelekwa Wizarani, kama ni Ofisa wa Polisi atapelekwa makao makuu n.k Halafu nafasi zao zinajazwa tena na manovisi!!! Gurudumu la maendeleo linaendelea kubiringishwa kinyumenyume!!

Hadi pale viongozi wetu watakapoelewa maana ya kuwa kiongozi, hapo ndipo tutakapoanza kuona mabadiliko! Semina ya Ngurdoto ilikuwa na lengo la kuwekana sawa miezi michache baadaye, WM analalamika kuwa semina haikuwaingia vichwani baadhi ya viongozi!! Uongozi ni kipaji na si elimu!! Uongozi mtu anazaliwa nao hafundishwi shuleni!! Aidha mtu ni kiongozi au siyo kiongozi! Sisi tunachanganya watawala, mameneja, mawaziri n.k na tunu ya uongozi!!!! Ni kwa sababu hiyo basi utakuta viongozi wa kweli bado wako nje ya mfumo!!!! Laiti wangepewa nafasi ya kuongoza! laiti Tanzania ingewatumia wana na mabinti wake ambao wamejaliwa vipaji vya uongozi bila ya kujali vyama vyao!!!

No comments:

Post a Comment