Wednesday, June 10, 2009

ajali ya moto yaunguza wanne moro.

Watu wanne wa familia moja wameungua vibaya kwa moto baada ya nyumba waliyokuwa wakiishi kuunguzwa kwa moto huku wao wakiwa ndani wamelala usiku wa saa tisa huko Mikese mkoani Morogoro.

Watu hao wa familia moja walioungua na moto ni mzee wa familia hiyo, mkewe , mtoto wao wa kiume pamoja na mjukuu wao mwenye umri wa miaka minne wote wamelazwa wakiwa mahututi katika hospitali ya mkoa wa Morogoro.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro Bw. Thobias Andengeye amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na amesema watu hao walifanyiwa kitendo hicho cha kinyama majira ya saa tisa za usiku wakiwa wamelala kwenye nyumba hiyo.

Amesema kuwa katika uchunguzi wa haraka wa polisi umebaini kwamba watu walichoma moto nyumba hiyo.

Watu waliofanya kitendo hicho hawajabainika na polisi ipo kwenye msako mkali kuwatafuta watu hao na ulinzi umetawala kwenye kijiji hicho huku msako wa nyumba hadi nyumba ukifanyika .

Kwa mujibu wa maelezo ya waathirika hao mtoto wa kiume wa familia hiyo aliyetambulika kwa jina la Rajabu Shaban ,30 amesema kuwa walikuwa wamelala ndani na mara waliona kama moshi umezingira nyumba hiyo lakini wao awali walijua labda kuni zilikuwa zinatoa moshi kwenye jiko ambalo liko ndani kwa ajili ya kujikinga na ubaridi.

Dakika zilivyozidi kuongezeka ndipo moshi huo ulipozingira nyumba nzima na kubaini kuwa nyumba yao ilikuwa imewashwa moto.

Kijana huyo alisema kuwa wakati anajitayarisha aende akawaamshe wazee wake hao moto ulishazingira nyumba yote na ingawa alifanikiwa kuwaamsha wazee wake lakini tayari walishaanza kuungua kwa kuwa nyumba nzima ilikuwa imeishapamba moto.

Kijana huyo alisema kuwa wakati anajitayarisha aende akawaamshe wazee wake hao moto ulishazingira nyumba yote na ingawa alifanikiwa kuwaamsha wazee wake lakini tayari walishaanza kuungua kwa kuwa nyumba nzima ilikuwa imeishapamba moto.

Amesema watu wasiojulikana walikuja nyumbani hapo na kuiunguza nyumba hiyo na kisha kukimbia na kusababisha kuteketea kwa mali zilizokuwemo ndani humo yakiwemo mazao, kuku na pesa shilingi elfu 30.
Sababu ya watu kuja kuunguza moto nyumba hiyo bado haijafahamika.

No comments:

Post a Comment