Wednesday, July 8, 2009

Maiti nane za ajali ya ndege ya Yemenair zaokotwa pwani ya Tanzania.

Miili ya watu wanane inayosadikiwa kuwa miongoni mwa watu 154 waliokuwamo kwenye ndege ya Shirika la Yemen iliyoanguka kwenye Bahari ya Hindi takriban wiki moja na nusu iliyopita, imeopolewa kwenye pwani ya kisiwa cha Mafia mkoani Pwani.

Mkuu wa wilaya ya Mafia, Manzie Mangochie aliwaambia waandishi wa habari kuwa wavuvi waliiona miili hiyo ikielea na ndipo walipoanza harakati za kuiopoa.

“Miili hiyo iliopolewa Jumatatu na wavuvi kwenye Bahari ya Hindi, hususan katika visiwa vya Juani, Gibondo na Mlali,” alisema Mangochie.

Alifafanua kuwa miili sita kati ya hiyo ni ya wanaume na miwili ikiwa ni ya wanawake na kwamba miili mingi ni ya watu wanaoonekana wana asili ya Bara la Ulaya na michache ni watu wanaoonekana kuwa na asili ya Afrika.

“Tayari tumeanzisha operesheni ya kutafuta miili mingine kwa ajili kuiopoa kwa sababu tuna matumaini ya kupata miili zaidi,” alisema.

Alisema miili ya watu wenye asili ya Afrika iliokotwa pwani ya kisiwa cha Mlali kilichopo jirani kidogo na kijiji cha Jimbo wilayani humo.

“Tumeopoa pia miili ya watoto wawili; mvulana na msichana mmoja tumeihifadhi ili kusubiri taratibu za kiuchunguzi na mchakato wa kutambua utaifa wao,” alisema Mangochie.

Mangochie, ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, alisema tayari wameshatoa taarifa katika ofisi za ubalozi wa Ufaransa nchini Tanzania.

“Balozi ameahidi kuja hapa haraka iwezekanavyo kwa ajili ya kuona na ikiwezekana kutambua baadhi ya miili iliyoopolewa,” alisema Mangochie.

“Pia tumewasiliana na Dar es Salaam control tower (mnara wa kuongozea vyombo vya usafiri majini) kuhusu tukio hili. Ni matumaini yangu kuwa wataisambaza taarifa hii katika nchi wanazotoka marehemu hawa, ikiwamo Comoro ili operesheni zao za kutafuta miili hiyo zifike hadi huku,” alisema Mangochie.

Alisema baada ya mwili wa kwanza kuopolewa na wanakijiji, taarifa zilifikishwa katika ofisi za mkuu wa wilaya na watu wengine katika kituo cha Marine Park wilayani humo ili kuimarisha msako zaidi wa miili katika maeneo iliyoopolewa.

“Baada ya hapo, Mafia Marine Park ilitoa boti na vifaa vingine ambavyo vilisaidia kutafuta na kuopoa miili zaidi ya marehemu hao,” alisema Mangochie.
Mangochie alisema operesheni yao itakuwa na manufaa kwa sababu inasadikiwa kuwa miili hiyo ni ya mwanzo kuopolewa tangu kuanguka na kuzama kwa ndege hiyo takriban wiki moja na nusu iliyopita.
“Tumewaomba wavuvi wote wilayani hapa kutoa taarifa za kuonekana au kuopolewa kwa mwili wowote wa marehemu kwa sababu inaweza ikawa ni miongoni mwa abiria waliokuwamo katika ndege hiyo ya Shirika la Yemen,” alisisitiza Mangochie.


Juhudi za Mwananchi kumpata Kamanda wa Polisi, mkoani Pwani, Mwakyoma hazikufanikiwa.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alithibitisha kuopolewa kwa miili hiyo, lakini alikataa kutoa maelezo zaidi kwa kile alichosema tukio hilo limetokea nje ya eneo lake la kazi.


“Mtafute Kamanda Mwakyoma kwa kuwa ndiye anaongoza hiyo operesheni... mimi naogopa kuzungumzia tukio lililotokea nje ya eneo langu la kazi,” alisema Kamanda Kova.

Ndege ya abiria aina ya Airbus 310 ya Shirika la Yemen ilianguka asubuhi ya Juni 30 kwenye Bahari ya Hindi ikielekea Comoro kutoka Paris, Ufaransa kupita Yemen ikiwa na abiria 154 ambao 143 walikuwa abiria huku 11 wakiwa wafanyakazi.

No comments:

Post a Comment