Wednesday, January 6, 2010

Meli ya abiria yazimika-ziwa victoria

Meliya Mv Butiama iliyokuwa ikisafirisha abiria kutoka Mwanza kwenda kisiwani Ukerewe imezimika katika Ziwa Victoria na kusababisha hofu kwa abiria zaidi ya 200 waliokuwa wakisafiri na meli hiyo.

Akizungumza na mwandishi wetu kwa njia ya simu mmoja wa abiria aliyekuwa kwenye meli hiyo, Wilhem Mulinda alisema kuwa meli hiyo ilizimika injini zote mbili wakiwa karibu na eneo la Makobe.


"Tuliondoka Mwanza saa 4:18 asubuhi na saa moja baada ya kuondoka hapo injini za meli zilizimika ghafla hivyo ikashindwa kuendelea na safari," alisema Mulinda.

Alisema kutokana na hali hiyo wamekuwa wakiambiwa kuwa wanakwenda kuchukuliwa na meli nyingine, lakini tangu asubuhi hadi saa 8:43 mchana hakuna meli yoyote iliyokwenda kuwachukua.

"Sasa hivi meli inapigwa na upepo kutoka sehemu za Kakobe tunaelekea maeneo ya Igombe na hatujui hatima yetu ingawa tumeambiwa kuwa kuna meli nyingine inakuja kutuchukua, alisema jana Mulinda.

Habari zaidi zilisema abiria waliokuwa ndani ya meli hiyo walikuwa wengi zaidi ya uwezo wake hivyo kusababisha, baadhi yao kukosa sehemu ya kukaa baada ya meli hiyo kuzimika.

"Abiria walioko ndani ya meli ni wengi hali ambayo imesababisha baadhi ya watu kukosa sehemu ya kukaa baada ya meli hiyo kukwama," ilidai taarifa hiyo.

Habari zilizopatikana jijini Mwanza zinadai kuwa meli hiyo ilikuwa na hitilafu kwenye injini, lakini iliruhusiwa kusafirisha abiria.

Uongozi wa kampuni ya meli hiyo ulipofuatwa kwa ajili ya kuzungumzia juu ya mkasa huo, ulikataa kuzungumza lolote.
Jeshi la Polisi mkoani Mwanza limethibitisha kuzimika kwa meli hiyo ziwani na kuahidi kutoa taarifa zaidi baadaye.


Ofisa Upelelezi Mkoa wa Mwanza, Deusdedith Nsimeki alisema hawezi kuzungumza lolote wakati huo, kwa vile alikuwa akielekea Igombe ambako meli hiyo inaelekea baada ya kusukumwa na upepo.

"Siwezi kuongea lolote sasa hivi wakati watu wanataka kufa ziwani; ninaelekea maeneo ya Igombe kuangalia jinsi gani tunaweza kusaidia kuwaokoa abiria hao," alisema Nsimeki.

Hata hivyo, habari zilizotufikia jana jioni zimeeleza kuwa baadaye meli hiyo ilifanyiwa matengenezo na kutengemaa kisha kuendelea na safari hadi Nansio, Ukerewe.

No comments:

Post a Comment