Friday, January 22, 2010

Ngeleja 'amfukuzisha kazi' mlinzi wa ATM

Pascal Mnaku, mlinzi wa kampuni ya Ultimate Security aliyepambana na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, kwenye mashine ya kuchukulia fedha (ATM) jijini Dar es Salaam, amefukuzwa kazi na muajiri wake.

Mnaku alijikuta kwenye mpambano mkali na waziri huyo baada ya kumtaka asogee pembeni ya mashine hiyo ya Standard Chartered ili kupisha wateja wengine baada ya Ngeleja kuonekana akitumia muda mwingi kuongea na simu akiwa ndani ya chumba cha mashine hiyo.

Kwa mujibu wa habari tulizozipata kutoka Ultimate na kuthibitishwa na Mnaku, uamuzi wa kumfukuza kazi ulitolewa mara baada ya kikao cha nidhamu cha kampuni hiyo kilichofanyika jana kuanzia saa 4:00 asubuhi hadi jioni kwenye ofisi za Ultimate.

"Ni kweli nimefukuzwa kazi na hivi ninavyoongea na wewe ndio nimetoka katika kikao cha nidhamu na uamuzi uliofikiwa ndio huo,"alisema mlinzi huyo ambaye hakutetereka wakati Waziri Ngeleja alipohoji kama anamfahamu ni nani wakati akitakiwa kutoka kwenye ATM.

"Na hii ni kutokana na kitendo changu cha kumtaka Waziri Ngeleja awapishe wateja wengine kwenye ATM," alilalamika Mnaku.

No comments:

Post a Comment