Thursday, February 25, 2010

Waziri Wassira apandishwa kizimbani

Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wassira jana alipandishwa kizimbani na kujitetea katika kesi ya madai ya Sh190 milioni inayomkabili.

Wassira anadaiwa fedha hiyo na mkurugenzi wa kampuni ya vifaa vya ujenzi ya Cargo Building, Andrew Ngai kama fidia ya uzalilishaji baada ya kushindwa kesi ya wizi na madai aliyoifungulia kampuni hiyo mwaka 1999.

Katika kesi hiyo namba 211 ya 1999 aliyoifungua katika Mahakama ya Kinondoni, Wassira alitaka Ngai amlipe Sh 6milioni kutokana na madai kuwa aliibiwa vigae vyake kupitia kampuni ya Ngai.

Hata hivyo mahakama hiyo ilitupilia mbali kesi hiyo baada ya kubaini kuwa siyo kweli na baadaye Ngai kufungua kesi ya madai namba 24, 2008 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kudai fidia ya Sh190 milioni.


Jana waziri Wassira aliongozwa na wakili wake Gaspar Nyika kutoa utetezi wake mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Liad Chamshama.

Waziri Wassira ambaye anamiliki Kampuni ya Siza Cold Storage alidai mahakamani hapo kuwa anamfahamu Ngai kuwa ni mkurugenzi wa kampuni ya vifaa vya ujenzi ,Cargo Building ambayo ilikuwa jirani na mahali alipokuwa akijenga nyumba yake ya biashara maeneo ya Msasani.


Akizungumza kwa kujiamini, Wassira alidai kuwa mwaka 1999, aliagiza vigae 2000 kutoka Afrika Kusini vyenye thamani kati ya Sh7milioni au 8 milioni na kuiomba kampuni ya Ngai imsaidie kuvihifadhi.

Aliendelea kuieleza mahakama kuwa alipokuwa anachukua vigae hivyo, aliacha vigae 600 na kofia zake lakini, havikupatikana tena hadi jana.

Nilipovihitaji vikawa havipo, nikaenda kwa Ngai ili aingilie kati vigae vyangu vipatikane, akasema atashughulikia na kweli alimwandikia barua mkurugenzi mwenzie Mahinya ambaye alieleza kwa maandishi vigae hivyo viliuzwa na fedha zikatumika kwa matumizi ya kampuni yake,Waziri Wassira aliieleza mahakama.

Aliongeza kuwa baada ya kufuatilia kwa muda mrefu akawa hana cha kufanya hivyo akatoa taarifa kituo cha polisi Oysterbay kwa kuwa kesi hiyo ilikuwa na sura mbili; wizi na madai.

Waziri Wassira aliendelea kudai mahakamani hapo kuwa katika kesi ya madai aliyoifungua mahakama ya Kinondoni, alishindwa na Ngai alimweleza kuwa atakata rufaa maana hakuamini kama watashinda kesi hiyo.

No comments:

Post a Comment