Friday, May 7, 2010

Serikali ilinde ajira za wananchi wake-Mwinyi

Siku mbili baada ya Rais Jakaya Kikwete kutoa hotuba kali na maagizo ya kutimua wafanyakazi wote ambao wangeitikia tangazo la mgomo lililotolewa na Tucta, Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi amesema serikali inatakiwa kulinda ajira za wananchi wake ili kudumisha amani.Rais Kikwete, akizungumza na wazee wa Dar es salaam kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee Jumatatu iliyopita, alisema mgomo huo ulioandaliwa na Tucta ni batili na kwamba, yeyote ambaye angehusika, angechukuliwa hatua za kisheria; ikiwa ni pamoja na nguvu ya polisi kutumika kuwazuia watakaoingia mitaani kuandamana.

Katika hotupa yake Kikwete alisema viongozi wa Tucta kuwa ni wazandiki, waongo, wanafiki na wafitini kwa kuwa wanakwenda kinyume na makubaliano yao na serikali.

Lakini Mzee Mwinyi alionyesha mtazamo tofauti jana katika hafla ya chakula cha mchana iliyoandaliwa na Shule ya Kimataifa ya Wavulana ya Feza, ambako alitoa somo fupi la dhima ya utu.

"Taasisi au nchi yoyote ambayo itakuwa haiheshimu utu wa wananchi wake, itakuwa inajichimbia kaburi," alisema Mwinyi kwenye hafla hiyo ambayo pia ilihudhuriwa na mtoto wa mfalme wa Norway, Haakon Magnus na baadhi ya viongozi wa nchi mbalimbali.

"Ni lazima kwa serikali yoyote ile kuwalinda watu wake na si kufanya uadui kati yake na wananchi.
Serikali yoyote duniani ni lazima ilinde ajira za wananchi wake ili iweze kudumisha amani na kuheshimu utu wa raia wake.

"Hotuba ya Rais Kikwete ilitafsiriwa kuwa ni ya vitisho na ambayo ilitolewa bila ya ushahidi wa kutosha kutoka pande zote mbili kuhusu maendeleo ya mazungumzo baina ya serikali na Tucta, ambayo ilieleza baadaye kuwa rais alipaswa kwanza kusikiliza viongozi wa shirikisho hilo badala ya kusikiliza watendaji wa serikali pekee.

Mgomo huo ambao ulipangwa kuanza Mei 5, umesogezwa mbele hadi baada ya Mei 8, siku ambayo serikali na Tucta watakutana kujadili suala la kima cha chini cha mshahara wa sekta ya umma, suala ambalo hadi sasa pande zote hazijafikia muafaka.

Mbali na haki ya ajira, Mwinyi pia alisema haki ya kuishi lazima ilindwe na serikali ili kuweza kudumisha amani na kuheshimu utu wa watu wake.

“Vitu kama uhuru wa kujieleza, kusali, mawasiliano lazima vipewe ruksa, lakini pia ajira na kuishi, haki hizi lazima zilindwe na serikali,” alisema Mwinyi.

Kauli hiyo ya Mwinyi imekuja wakati kukiwa bado na kutoelewana baina ya serikali na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta) lililositisha mgomo uliopangwa kuanza Mei tano mwaka huu, baada ya Rais Jakaya Kikwete kutoa hotuba kali ambayo wadau mbalimbali walisema ilikuwa imejaa vitisho.Mbali na hayo Mwinyi alisema:

“Shule ya Feza ni nzuri sana, ni nzuri kwa sababu ina walimu wazuri na hata wanafunzi wake ni wazuri, hata katika matokeo yake imekuwa ikifanya vizuri na kuwa ndani ya shule tano bora.”

Kabla ya kutoa hotuba yake, baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo walieleza kwa nyakati tofauti juu ya maana ya utu kutokana na mafunzo waliyopata kutoka kwa viongozi hao wa vijana wa dunia.

Watu mbalimbali, akiwemo mtoto huyo wa mfalme wa Norway walikuwa wakihamasika na kuwashangilia wanafunzi hao walipookuwa wanaeleza maana ya utu, umuhimu wa kuheshimu utu wa mtu na athari zake endapo hautaheshimiwa.

Prince Haakon aliwaambia vijana hao ni muhimu kuheshimu utu na kujiamini kwa kuwa wao ndiyo watakaoweza kuifanya Afrika na dunia kwa ujula kuwa mahala pazuri na salama pakuishi.

Baadhi ya wanafunzi hao wakizungumza mbele ya Mzee Mwinyi walisema "utu ni kuheshimiana baina ya mtu na mtu; kusema ni sisi na si ni mimi, kujiuliza nimetoa nini na siyo nimepokea nini".

Wengine pia walisema, kujilimbikizia mali nyingi si utu na kuwa hata mtu huyo aliyejilimbikizia mali wakati anazungukwa na watu masikini haishi maisha ya amani kwa kuwa wale wasio nacho nao watakuwa wakifanya kila liwezekanalo kupata mali za mtu huyo tajiri.

No comments:

Post a Comment