Thursday, June 10, 2010

mambo yaiva sauzi.

(Mashabiki 10 Argentina watimuliwa
Frank Sanga, Johannesburg)


Ukiachilia mbali kwa Mashabiki 10 wa Argentina kurudishwa kwao kwa nguvu ni shamrashamra tupu ndizo zimetawala tangu kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Oliver Tambo jijini Jburg huku mashabiki wengi wakionekana kuwa na tarumbeta zao, vuvuzela, lakini timu ya taifa ya Afrika Kusini 'Bafana Bafana' imefanya maandamano ya kuungwa mkono.

Wageni ambao wamekuwa wakitoka katika nchi mbalimbali wamejikuta wakiwa katika wakati mgumu kutokana na vuvuzela kupigwa mfululizo uwanjani hapo huku kukiwa na ulinzi mkali, lakini bila usumbufu wowote kwa mashabiki.

"Najisikia raha kuwa hapa Afrika Kusini, safari kutoka Argentina imekuwa ndefu kiasi, nakwambia lazima tuchukue ubingwa mwaka huu," alisema shabiki wa nchi hiyo aliyejulikana kwa jina la Juan akiwa amembatana na mwanaye mwenye umri wa miaka sita.

Juan, sawa na mwanawe walikuwa wamevaa jezi za timu ya taifa ya Argentina huku wakiwa wanapeperusha bendera yao tangu waliposhuka kwenye ndege jana asubuhi.

Zaidi ya mashabiki wanaokadiriwa kufikia 2,000 walikuwa uwanjani hapo wakiwa wamevaa jezi za timu zao; wengine wakitua na wengine wakisubiri wenyeji wao, lakini nafasi kubwa ilichukuliwa na matarumbeta hayo ambayo yameugeuza uwanja huo wa kimataifa wa ndege kuonekana kama uwanja wa soka.

Mashabiki wengi waliokuwa wametawala uwanjani hapo jana ni wa Argentina, Mexico na Slovakia ambao walionekana kwenye makundi ya watu zaidi ya 50, huku wakipiga picha na kupiga mavuvuzela na kupeperusha bendera za nchi zao.

Katika tukio jingine, mashabiki 10 wa Argentina wamerudishwa kwao mara baada ya kufika uwanja wa ndege juzi kutokana na kuwa na historia ya uhuni viwanjani.

Redio maarufu ya mjini Jburg, Talk 702 ilitangaza jana kuwa mashabiki hao walirudishwa mara baada ya kufika uwanjani hapo na kugunduliwa na mtambo wa kompyuta kuwa wana historia ya kuwa na vurugu viwanjani.

Kila shabiki anayefika katika uwanja wa Oliver Tambo amekuwa akitambuliwa na kompyuta hiyo na wale wenye matukio ya uhalifu wamekuwa wakirudishwa.

Wakati huohuo, wachezaji wa Bafana Bafana jana walipita katika mji wa Sandton huku mashabiki wakiwa wamejipanga barabarani kwa ajili ya kutafuta kuungwa mkono kwa ajili ya fainali hizo za Kombe la Dunia.

Hilo lilikuwa ni tukio kwa ajili ya kuipa timu hiyo morali na kuwashirikisha mashabiki wa Afrika Kusini kuiunga mkono timu yao.

No comments:

Post a Comment