Thursday, July 1, 2010

Wazee wote kulipwa pesa ya kujikimu kimaisha.

Serikali iko katika hatua za mwisho kutekeleza majaribio ya mpango wa pensheni kwa wazee wote nchini ili kuwazezesha kujikimu mahitaji yao muhimu ya kila siku.

Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Profesa Juma Kapuya alisema hayo jana wakati wa uzinduzi wa taarifa ya utafiti wa Mpango wa Pensheni kwa Wazee Wote.

“Tanzania sio nchi tajiri, lakini serikali tumeona hatushindwi kuwahudumia wazee kwa kuwapa fedha za kijikimu kwa kipindi tutakachokuwa tumekipanga. Tunaamini uendelevu katika kuwapa fedha hizi kutawawezesha hata wale wanaoishi vijijini bila kujali wataweza kufurahia mazingira wanayoishi na kutambua mchango wao katika nchi yao,” alisema Kapuya.

Kapuya alisema serikali kwa kushirikiana na wabia mbalimbali katika maendeleo inafanya tafiti mbalimbali ili kuona namna ya kupanua wigo wa huduma za hifadhi ya jamii, kuwafikia wananchi wengi ikiwa ni pamoja na wazee.


“Ripoti ninayoizindua leo ni sehemu ya juhudi za serikali katika kutimiza azma ya kupanua wigo kwa kutoa hifadhi katika jamii yetu, taarifa hii ambayo imekuwa na mapendekezo kadha wa kadha imeifanya serikali kuona kuwa hakuna sababu ya kusuburi tafiti nyingine bali kuifanyia kazi," alisema Kapuya.

“Ili kuthibitisha hilo kwa sasa serikali yetu iko katika hatua za mwisho kwa kushirikiana na Shirika la Misaada la Uingereza na tutahakikisha kuwa mara baada ya mazungumzo kukamilika, utekelezaji wake utaanza kwa kutoa pensheni kwa wazee wote,” alisema Kapuya.

Alisema Tanzania inakadiriwa kuwa na wazee wapatao milioni mbili ambayo ni sawa na asilimia nne ya wananchi wote na kuwa wamekuwa wakiishi katika mazingira magumu.

Alisema serikali imeamua kutilia maanani utafiti huo ili kuangalia uwezekano wa kuwapatia pensheni wazee wenye umri wa kuanzia miaka 60 na kuendelea bila kujali kuwa walikuwa watumishi serikalini na kwamba lengo ni kuwawezesha kupata mahitaji muhimu.

“Kuna idadi ndogo ya watu wanaofaidika na utaratibu wa hifadhi ya jamii ambao ni chini ya asilimia nne ya nguvu kazi. Idadi hii ndogo inatokana na kukua kwa sekta isiyo rasmi na kukosekana kwa sheria na mipango ya kuwajumuisha watu walio katika sekta isiyo rasmi,” alisema.

Alisema kuwa taarifa ya utafiti inaonyesha kuwa mfumo wa asili ya hifadhi ambao kwa miaka mingi umekuwa ukitumika kuwapatia mahitaji muhimu wazee, unadhoofika kwa kasi na kuwaacha wengi pasipo kinga yoyote.
Kapuya alisema watumishi wa umma wamekuwa wakiendeleza vitendo vya ufisadi mara baada ya muda wao wa kustaafu kukaribia kwa kuwa wamekuwa hawana uhakika wa kuishi baada ya kustaafu.

“Ufisadi umekuwa ukifanyika kwa watunishi wa umma wakati ambaho aliyekaribia kustaafu anakuwa hana uhakika wa kuishi baada ya kustaafu, hata wengine wamediriki kupunguza umri wakati kipindi chake cha kustaafu kinapokaribia. Na hii tunaishuhudia, unaweza ukaona mzee kaishiwa nguvu lakini haachii kazi kwa vijana,” alisema Kapuya.
Vilevile alisema ipo mifuko mitano ya hifadhi ya jamii ambayo imekuwa ikitumika katika masuala ya pensheni kwa sekta mbalimbali za serikali na sekta binafsi ambayo ni NSSF, PPF, PSPF, LAPF, NHIF na GEPF, lakini akasema haitoshi.

Aliongeza kuwa serikali imeanza kuongeza mipango ya utekelezaji wa huduma kwa jamii kwa kupitia Tasaf, Mpango wa Misaada kwa walemavu (PWDs) na Mfuko wa misaada kwa watoto waishi katika mazingira magumu ili kuhakikisha makundi yenye mahitaji muhimu yanafikiwa.

Awali akiwasilisha ripoti Mtafiti kutoka Shirika la Kimataifa la Kusaidia Wazee (Help Age International), Stephen Barrett alisema asilimia 75 wa wazee walioofikia miaka 60 na kuendelea wamekuwa wakiendelea kufanya kazi kulingana na umasikini wa familia zao.

Alisema kulingana na mahitaji ya uzeeni wazee wamekuwa wakipoteza uhai wao mapema kwa kukosa mahitaji muhimu na maisha yao yamekuwa yakikabiliwa na magonjwa sugu yanayohitaji uangalizi mkubwa.


“Kuna haja ya serikali kuangalia umri wa wazee ambao hata baada ya miaka 60 wamekuwa wakiendelea kufanya kazi ili waweze kupata mahitaji yao muhimu kulingana na umasikini wao, ili kuweza kuepuka kuwapoteza wazee ambao ni hazina kwa kizazi kijacho,” alisema Barrett.

Katika hatua nyingine wazee waliwasilisha mada yao, wakiishukuru serikali kufikia hatua hiyo kwa kuwa wazee wamekuwa waathirika wakubwa kwa kubeba mzigo wa kulea yatima wanaoachwa na wazazi wao kutokana na ugonjwa wa Ukimwi.

“Asilimia 50 ya watoto yatima hapa nchini wamekuwa wakilelewa na wazee, wakati wazee wanahitaji nao kulelewa, huu mzigo sio wetu. Lakini kwa kuanzisha pensheni kwa wazee kutakuwa na nafuu kubwa ya kuweza kuwalea wajukuu wetu,” alisema mtoa mada, Mama Kokupima.

No comments:

Post a Comment