Thursday, November 3, 2011

Vurugu Arusha na Mwanza

Vurugu kubwa zimetokea jana katika majiji ya Arusha na Mwanza kiasi cha kuwalazimu polisi kutumia mabiomu ya machozi na baadhi ya watu kutiwa nguvuni.

Jana asubuhi jijini Arusha, watumishi wa daladala zinazojulikana huko kama vifodi, waliitisha mgomo kulaani kile walichokiita unyanyasaji wa polisi hatua iliyowalazimu askari hao kuingilia kati na kuwatia mbaroni zaidi ya watu 30.

Mgomo huo ulianza majira ya saa mbili asubuhi na kudumu hadi saa 5:00 asubuhi.
Pia polisi na askari wa Magereza walikuwa na kibarua kizito kuwadhibiti wafuasi wa Chadema kwenda katika Gereza la Kisongo kumwona Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema.


Polisi waliweka ulinzi mkali wakiwazuia na kuwahoji watu wote waliokuwa wakielekea njia ya Kisongo liliko Gereza hilo Kuu la Mkoa wa Arusha ambako Lema yuko mahabusu.

Wafuasi hao wa Chadema walikuwa wanataka kwenda kumwona mbunge huyo katika utaratibu wa kawaida wa kuwaona wafungwa na mahabusu katika gereza hilo siku za Jumatano, Jumamosi na Jumapili.

Baadhi ya wananchi waliofanikiwa kupenya kupitia njia za vichochoroni na kufika gerezani hapo, walikumbana na kizingiti kingine cha askari Magereza ambao waliwazuia kumwona mbunge huyo kwa madai idadi ya watu inayotakiwa kumwona ilishatimia.

Ofisa Magereza mwenye cheo cha mkaguzi msaidizi, aliyekuwa amevaa beji yenye jina la J. Mmari alizungumza na wananchi hao kwa niaba ya mkuu wa gereza hilo akisema sheria inaelekeza kuwa siku ya Jumatano wanaoruhusiwa kumtembelea mtuhumiwa ni mawakili wake na wageni wasiozidi watatu, lakini kwa busara uongozi wa gereza uliamua kuruhusu watu zaidi.

“Mpaka sasa walioingia kumwona Lema wamezidi na hatuwezi kuendelea kuruhusu kwani tangu saa 2:00 asubuhi Mheshimiwa ametembelewa na idadi kubwa na anaongea nao kwa zaidi ya dakika kila kundi. Tafadhalini wengine njooni Jumamosi na Jumapili,” alisema Mmari.

Kauli hiyo iliamsha jazba na hasira za vijana walioanza kutoa maneno makali na kumlazimu mwenyekiti wa Bavicha Wilaya ya Arumeru, Joshua Nassari kuwatuliza.

No comments:

Post a Comment