Kampuni kandarasi ya Wartsila Tanzania imevunja mkataba wa kuendesha na kutengeneza mitambo ya megawati 100 ya kuzalisha umeme ya kampuni ya Independent Power Tanzania Ltd (IPTL).
Kuvunjwa kwa mkataba huo, kumekuja baada ya IPTL kushindwa kuilipa fedha Wartsila kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia Aprili 2007 hadi February 2009.
Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa jana katika vyombo vya habari na Wartsila, inasema iliingia mkataba kuendesha na kutengeneza mitambo hiyo, mwaka 2002.
“Tunasikitika kutangaza kuwa Wartsila imevunja mkataba wa kuendesha na kutengeneza mitambo ya IPTL ya megawati 100.
“Hatua hii imekuja baada ya IPTL kushindwa kutulipa fedha kwa mujibu wa makubaliano tuliokubalina kwa kipindi cha kuanzia Aprili 2007 hadi Februari 2009,” ilisema sehemu ya tangazo hilo.
Hata hivyo, uongozi wa Wartsila jana haukuwa tayari kueleza kiasi cha fedha inachodai.
Lakini kwa mujibu wa tangazo hilo, Wartsila kwa kipindi chote ilikuwa ikiendesha mitambo hiyo kwa kutumia fedha zake na kwamba ilifanya hivyo kwa ajili ya maslahi ya taifa na wadau wake.
“IPTL imeshindwa kufanya malipo ya kila mwezi kwa Wartsila kulingana na makubaliano ya mkataba tulioafikina mwaka 2007 wa kuendesha na kutengeneza mitambo, chini ya Shirika la Umeme Tanzania(Tanesco),” ilisema tangazo hilo.
Kutokana na hali hiyo, pamoja na mambo mengine Wartsila inawaomba radhi watanzania kwa uamuzi uliofikiwa na kwamba imeamua kuwaondoa wafanyakazi wake wote waliokuwepo katika mitambo hiyo, iliyopo Tegeta jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa tangazo hilo, inasema imeacha mitambo hiyo kumi yenye uwezo wa kutoa megawati 10 kila mmoja ikiwa katika ubora wake na yenye uwezo wa kuzalisha umeme wakati wowote.
Uongozi wa IPTL jana ulipotafutwa kwa njia ya simu haukuwa tayari kuzungumzia suala hilo.“Muda huu, majira ya saa 7:00 mchana hakuna kiongozi yoyote wa IPTL hapa ofisini na pia hawatorudi kabisa,” alijibu dada mmoja wa mapokezi wa IPTL.Katika hatua nyingine,
Wartsila imesema itaendelea kuendesha na kutengeneza mitambo ya kufua umeme ya Ubungo na Tegeta inayomilikiwa na Tanesco kwa mujibu wa mkataba uliopo.
Thursday, May 6, 2010
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment