Thursday, March 12, 2009

Aliyempiga mzee ruksa kofi aeleza sababu.

Kijana anayeshikiliwa kutokana na kumpiga kofi Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi amepelekwa hospitalini kupimwa akili huku Polisi ikiendelea kuchunguza kama anahusika na kikundi chochote cha wanaharakati wenye msimamo mkali.

Wakati hatua hiyo ikichukuliwa, taasisi na watu mbalimbali wamelaani kitendo hicho cha kumpiga Rais mstaafu na kusema ni kinyume na maadili ya Watanzania. Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba kijana huyo, Ibrahim Said (26) aliiambia Polisi kuwa alifanya hivyo kutokana na kuchukizwa na hotuba zinazosisitiza Waislamu kushirikiana na Wakristo.

Kova alisema kijana huyo alidai kwamba aliamua kumpiga kiongozi huyo mstaafu kwa sababu hakubaliani na hotuba za viongozi wa Kiislamu zinazosisitiza Waislamu na Wakristo kushirikiana katika kuadhimisha sikukuu za kidini kama vile Maulid, Idd (kwa Waislamu), Pasaka na Krismasi (Wakristo).

Kwa mujibu wa Kova, Said alidai kuwa hakuwa na lengo lolote la kumdhuru Rais Mwinyi bali alikuwa akifikisha ujumbe kwa jamii. Kamanda Kova alisema alipohojiwa na Polisi, Said alisema anataka sikukuu za Kiislamu washerehekee kivyao na Wakristo washerehekee peke yao, wasilazimishwe kuwa na umoja.

Pia Said alidai anapinga matumizi ya kondomu kwa kuwa watu wakitumia kondomu, watakuwa wamehalalisha uzinifu kwa Waislamu. Kova alisema kutokana na kitendo cha Said kumpiga Rais Mwinyi aliyekuwa mgeni rasmi katika Baraza la Maulid lililofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam juzi saa 12 jioni, alipelekwa jana Muhimbili kabla ya kufikishwa leo mahakamani.

Daily News.

No comments:

Post a Comment