Monday, March 2, 2009

hali inapokuwa ngumu zaidi.

Mpenzi msomaji, hali ya uchumi inayoikumba dunia hivi sasa, taratibu imeanza kujipenyeza katika nchi zetu, na hakika, kama ndivyo, basi huku tuendako hali ni mbaya.

Hivi unaweza kuamini kuwa mtu yuko radhi ajidhalilishe ili mradi tu mkono uingie kinywani?

Hasa vijana wetu ndio wanaoonekana kufanya vituko ili waweze kujikimu kimaisha. Hebu sikia kituko hiki kisha baadaye unitumie maoni yako.

Jumapili iliyopita, nilisimuliwa kituko kimoja kilichotokea jana yake, Jumamosi sehemu ya temeke ambapo kijana mmoja aliamua kutembea uchi wa mnyama hadharani, tena kwa mbwembwe nyingi.

Kijana huyu(jina kapuni), ni mbeba mizigo kwa kutumia baiskeli. Ofisi yake kubwa ni kwenye vituo vya daladala ambako husubiri abiria wanaoshuka kwenye mabasi ili kama wanayo mizigo ya kubeba afanye kazi hiyo kwa ujira fulani. Ni baba mwenye mke na watoto wawili.

Kwa mujibu wa vijana wenzake wanaomfahamu kijana huyo, siku ya tukio alionekana akicheza kamari katika eneo moja la soko.

Wajua tena kamari ni pata potea. Akajitutumua lakini wapi

Kila akijaribu kucheza analambwa (zake zinaliwa). Mwishoni akapandwa na hasira na kuanza kugombana na mwenzake.

Jirani na alipokuwa akichezea kamari, walikuwepo vijana wenzake wakicheza mchezo wa pool table. Pia alikuwepo mmiliki wa pool table hiyo.

Mmiliki huyu kuona jamaa huyo anazusha ugomvi akamwambia, ``kama wewe ni jasiri na unahitaji sana hela, vua nguo utembee uchi wa mnyama umbali wa nusu kilomita(akamwelekeza mwisho wa umbali huo), halafu nitakupa sh.30,000/-``.

Kama vile ni sinema ya kuigiza, kijana yule aliamua kuchojoa nguo zake zote na kumkabidhi mweka dau yule. Walioshuhudia hawakuamini walidhani ni miugiza.

Jamaa huyo akaondoka zake, tena kwa mbwembwe nyingi kuelekea alikuelekezwa kwenda.
Alipita kwenye barabara ambayo hupita magari na watu wengi waenda kwa miguu.

Wakati huo ulikuwa muda wa saa tisa alasiri. Jamaa akaongoza njia na alipofikia usawa wa baa moja kandoni mwa baraba ile, akachepuka na kujitosa kwenye baa ile.
Wateja waliokuwepo wakabaki wameduwaa wakiona kama ni mzuka vile.

Mwenyewe akavuta kiti na kuagiza bia. Mhudumu alisita kidogo lakini jamaa akasisitiza ``nipe bia nina hela kibao hivi sasa``. Mhudumu ikabidi amletee bia. Huko nyuma mweka dau yule alikuwa akimfuatilia jamaa huyu huku akiwa ameshikilia nguo zake mkononi

Huku watu wakiendelea kujaa kumshangaa kijana yule, akawasili mweka dau na kumkabidhi nguo zile pamoja na 30,000/- . Kijana akavaa nguo zake, akalipa bia yake na kuishia zake huku watazamaji wakimsindikiza kwa macho. Ama kwa hakika, Maisha Ndivyo Yalivyo. Au siyo msomaji wangu.

Baada ya kusimulia kisa hiki, nilijiuliza maswali lukuki. Kwanza, kijana yule alikuwa na dhiki ya fedha kiasi cha kuafiki kudhalilika kwa kiwango kile?
Pili, jamii inayomzunguka itamuonaje? Familia yake je? Na tatu aliyetangaza dau lile la sh.30,000/- aliona kitendo kile ni sahihi kwa kumdhalilisha kijana mwenzie?

Kwanini kama aliona kijana huyu alikuwa anahitaji sana fedha asingemkopesha badala ya kumpa sharti lile baya ambalo ni kinyume na haki za binadamu? Angefanyiwa ndugu yake angeona ni sahihi? Ajabu nyingine ni kwamba, hata wale vijana wenzake waliokuwa naye walionekana kumshangilia eti kwa ujasiri ule wa kutembea akiwa mtupu.

Kama hata wenzake hao hawakemei hali au kitendo kile, nani atafanya kazi hiyo? Jamii yetu inakwenda wapi? Kwanini mambo haya yatokee wakati huu na hayakuwahi kufanyika hivyo, tena hadharani katika miaka ile walioishi mababu zetu?

Ukiona moshi unafukuta, ujue pale pana moto. Hivyo ni viashiria ambavyo yafaa viangaliwe kwa mapana ili kuziba ufa badala ya kusubiri kujenga ukuta. Au siyo msomaji wangu?

Kama hali inafikia hivi, tutazamie vituko zaidi huko tuendako. Mtu anaweza kuzidiwa kifedha akaamua hata kumweka mkewe rehani. Ebo! Unashangaa?
Mtu atakwambia eti kugusa siyo kuchukua. Lakini hata huko kugusa tayari si ni kishawishi tosha?

Ni mara ngapi tumesikia kwenye vyombo vya habari mtu anamwozesha bintiye mwanafunzi ili apate mahari kujikimu kimaisha. Wengine wanauza watoto wao kwa fedha taslimu.
Wengine wanawatuma kwenye ukahaba ili mradi walete fedha za matumizi. Hii ni hatari sana.

Tufanye nini sasa? Serikali na vyombo vinavyosimamia ustawi wa jamii yafaa vijipange kukabiliana na athari za kuyumba kwa uchumi duniani ambako kumeanza kujitokeza hivi sasa.

Inaonekana kama ni vichekesho lakini kama viashiria hivi vikiachwa viendelee, hadhi ya taifa letu ambayo tumeijenga kwa miaka mingi itaporomoka kwa muda mfupi. Tuzibe nyufa kuzuia kuta zisibomoke na hivyo kuligharimu taifa katika kuzijenga.

No comments:

Post a Comment