Thursday, April 23, 2009

Kimo ni kikwazo kwa Ngassa!!!

Kimo kifupi alichonacho winga mchachari wa klabu ya Yanga na timu ya taifa, Mrisho Ngassa, kimedaiwa ndicho kinachoifanya hadi sasa klabu ya West Ham ya Uingereza kushindwa kutoa majibu juu ya winga huyo. Hatahivyo, klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu nchini humo, inatarajiwa kutoa taarifa rasmi ya kufaulu au kufeli kwa mchezaji huyo Ijumaa. Wakala anayetambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Soka, FIFA, Yusuph Bakhresa, aliliambia gazeti hili kwa njia ya simu toka Uingereza kuwa, kimo alichonacho Ngassa ndicho ambacho hakijawaridhisha West Ham.

Bakhresa alisema kuwa, hata hivyo klabu hiyo iliyomuongezea muda zaidi wa majaribio winga huyo, imesema inaangalia namna ya kumchukua mchezaji huyo huku ikimjenga stamina amudu kucheza licha ya ufupi alionao. ``Mpaka sasa maendeleo ya Ngassa hapa West Ham ni mazuri ikiwa ni pamoja na kuwaridhisha kwa kasi, umiliki na umakini wake uwanjani, ila ufupi wake ndio umewapa kigugumizi klabu hiyo,`` alisema Bakhresa. Wakala huyo alisema ameelezwa kuwa tamko rasmi juu ya Ngassa litatolewa na West Ham, Ijumaa ambapo itafahamika kama amefeli au kufaulu kuichezea klabu hiyo inayoshiriki Ligi K uu ya Uingereza.


``Wamenieleza kwamba taarifa juu ya majaribio ya Ngassa watatoa Ijumaa na kushangaa kusikia huko nyumbani mnaripoti kuwa mchezaji huyu amefeli.`` Alisema na kuongeza kuwa hata kama Ngassa atafeli majaribio yake West Ham, bado ana nafasi kubwa kutua Fulham ambayo imeonyesha kuvutiwa na winga huyo na kumtaka kumchukua kama kweli wenzao watamuacha. Ngassa aliondoka nchini wiki mbili zilizopita kwenda Uingereza kwa ajili ya majaribio ya kucheza soka la kulipwa katika klabu hiyo ya West Ham na tayari imeripotiwa kuwa mchezaji huyo amefeli kitu kinachokanushwa kwa sasa.

Hatahivyo, Ngassa huenda ameshindwa kuonyesha kiwango kinachoridhisha na sio kimo kwani katika ligi mbalimbali za Ulaya kuna wachezaji wenye vimo vifupi lakini wanategemewa na timu zao kama akina Robinho, Roberto Carlos na wengineo.

SOURCE: Nipashe

No comments:

Post a Comment