Thursday, May 28, 2009

Barcelona Mabingwa wa Ulaya, Yaibanjua Manchester 2-0




Mabingwa wa Hispania Barcelona, wameliteka jiji la Roma usiku wa jana na kuwa mabingwa wapya wa ulaya kwa kuigaragaza Manchester United kwa kuifunga mabao 2-0.
Barcelona ikicheza kwa kujiamini sana na ikitandaza pasi fupi fupi za uhakika imefanikiwa kutwaa taji la ubingwa wa Ulaya kwa mara ya tatu katika historia yake baada ya kuwabanjua mabingwa watetezi Manchester United ya Uingereza kwa mabao 2-0.

Kocha wa Barcelona Josep Guardiola ameweka historia kwa kuwa kocha kijana kuliko wote kutwaa kombe la mabingwa wa ulaya.
Naye Kocha wa Manchester United, Alex Ferguson akiongea baada ya mechi alikiri kwamba Barcelona ilistahili kutwaa kombe hilo kutokana na uwezo mkubwa sana iliouonyesha leo kuliko timu yake ya Manchester.
"Kusema kweli tumefungwa na timu iliyokuwa bora sana zaidi yetu", alisema Ferguson.
Manchester United ilianza kipindi cha kwanza kwa kasi sana na kuitia ngome ya Barcelona katika mashaka makubwa kwa kosa kosa nyingi za Cristiano Ronaldo.
Manchester United ilinyamazishwa na kupoteza muelekeo kabisa katika mechi ya hiyo pale Samuel Eto'o alipoifungia Barcelona goli la kuongoza katika dakika ya 10 baada ya kuipangua ngome ya Manchester na kumuacha kipa wao akigaragara huku mpira ukitinga nyavuni.
Goli hilo liliifanya Manchester ianze kucheza bila mpangilio maalumu na kuanza kupoteza mpira mara kwa mara na kuipa nafasi Barcelona kuitawala mechi hiyo.
Goli hilo lilidumu hadi mapumziko na kuifanya Barca iende mapumziko ikiwa kifua mbele.Katika kipindi cha pili, pamoja na Alex Ferguson kuingiza vifaa vyake vyote uwanjani ili kuokoa jahazi lakini Barcelona ilikuwa bora zaidi ikicheza kwa kujiamini zaidi kwa pasi zake fupi fupi huku ikilisakama lango la Manchester.

Alikuwa ni Lionel Messi aliyehitimisha mazishi ya Manchester pale alipoifungia Barcelona goli la pili kwa kichwa safi katika dakika ya 70.Baada ya goli hilo Manchester iliendelea kucheza hovyo huku baadhi ya wachezaji wake kama Cristiano Ronaldo, Vidic na Scholes wakianza kuwacheza rafu hovyo zilizopelekea wapewe kadi za njano.

Nyota wa mechi alikuwa ni Andres Iniesta ambaye alicheza kwa ustadi mkubwa sana akiwaunganisha vyema washambuliaji wa Barcelona. Alikuwa ni Iniesta aliyemtengenezea Eto'o goli la kwanza.
Uwanja wa Stadio Olimpico uligubikwa na sherehe za mashabiki wa Barcelona baada ya refa wa mechi hiyo kupuliza kipyenga cha mwisho kilichoitangaza Barcelona mabingwa wapya wa ulaya.

No comments:

Post a Comment