Wednesday, May 20, 2009

kasi ya utupaji watoto wachanga yazidi kuongezeka Arusha.

Kasi ya utupaji wa watoto wachanga katika Manispaa ya Arusha imekuwa ikiongezeka kwa kasi kutokana na kuwa na idadi kubwa ya watoto wanaookotwa kila mwaka katika Manispaa hiyo.

Hayo yamebainika baada ya kufanyika kwa takwimu za kupata idadi ya watoto waliookotwa katika kipindi cha miaka minane katika kituo cha kulelea watoto cha Samaritan kilichopo Arusha.

Imegundulika kuwa toka mwaka 2002 hadi kufikia mwaka huu watoto 65 waliokotwa na kulelewa katika kituo hicho.

Mratibu wa Kituo hicho, Japhet Mmanyi amesema katika kipindi hicho wameweza kuokota idadi ya watoto hao na kuchukua jukumu la kuwalea watoto hao ambao hawana hatia yoyote.

Amesema watoto hao wameweza kuokotwa katika mazingira tofauti ikiwa ni pamoja na majalalani, misituni na hata barabarani na wengine kuachwa kwenye mabaa.

Ameongeza kuwa kuna baadhi ya wakina mama wanatupa watoto hao kwa sababu za kukosa uwezo wa kuwatunza watoto hao kutokana na kutelekezwa na waume zao waliowapa mimba hizo na sababu nyingine mbali mbali.

Kaimu Afisa Ustawi wa Jamii Arusha, Simba Panga amesema kuwa wakina mama walio wengi wamejenga dhana kuwa wanazaa watoto hao na kuwaweka barabarani kwa kudhani kuwa wataokotwa na wasamaria wema na kulelewa kitu ambacho kinasikitisha sana mkoani humo.

Amesema sheria kali zitekelezwe pindi mtu yoyote atakayepatikana anatupa mtoto ili kuweza kumaliza wimbi hilo la kuongeza kwa watoto wa mitaani wasiokuwa na hatia yoyote.

No comments:

Post a Comment