Wednesday, May 20, 2009

Akamatwa Uwanja wa Ndege Dar akiwa amemeza dawa za kulevya.

Kijana Paul Haule Komba amekamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere wa jijini Dar es Salaam, akiwa amemeza pipi za dawa za kulevya aina ya Cocaine.

Komba alikuwa amemeza zaidi ya pipi 80 za cocaine ambazo alikuwa amezihifadhi tumboni ili atakapofika salama aweze kufanya biashara hiyo haramu.

Kamishna wa Kudhibiti Madawa ya Kulevya nchini, Godfrey Nzowa alisema kijana huyo alikamatwa uwanjani hapo akiwa anatokea Brazil kupitia nchini Dubai.

Amesema kijana huyo alikuwa na pasipoti yake ya kusafiria iliyotolewa nchini iliyokuwa na namba AB 321311 ambayo aliweza kwenda nchi hizo na kubeba dawa hizo ili aingize nchini.

Amesema hadi jana kijana huyo waliweza kumtoa pipi alizokuwa amemeza zipatazo pipi 78 ambazo alizitoa kwa njia ya haja kubwa.

Amesema katika utafiti uliofanyika na wataalamu wa madawa hayo kijana huyo bado alikuwa na pipi nyingine kadhaa ambazo wanaendelea kumtoa.


Amesema watakapomaliza zoezi la kumtoa pipi hizo ataweza kuchukuliwa hatua ikiwemo na kujieleza kwa kina kama aliagizwa ama ni biashara yake mwenyewe.

Pia ataweza kufunguliwa mashitaka Mahakamani kwa kosa la kutaka kuingiza madawa hayo nchini kinyume cha sheria za nchi.

No comments:

Post a Comment