Sunday, May 24, 2009

Mbunge amvaa Dkt. Hosea mkutanoni.

Mbunge wa Jimbo la Kishapu kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),Bw.Fredy Mpendazoe juzi alimvaa Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU),Dkt. Edward Hosea kwa madai kuwa taasisi yake imedorora kutokana na upungufu uliomo ndani katiba ya nchi jambo linalohitaji marekebisho ya haraka.

Akichangia hoja kwenye Semina ya Wabunge kuhusu rushwa iliyofanyika Dar es Salaam, Bw. Mpendazoe, alisema kutokana na madaraka makubwa ya Rais kikatiba, anaweza kuteua marafiki zake ambao mamlaka husika kama TAKUKURU haziwezi kuwagusa inapobidi.

Alishauri wateule wa Rais kwa nafasi kama TAKUKURU, Usalama wa Taifa na Tume ya Maadili ya Viongozi, waidhinishwe kwanza na Bunge na Rais afanye kazi ya uteuzi tu.

Alitoa mfano wa Mkurugenzi wa TAKUKURU kushindwa kuwashughulikia baadhi wateule wa Rais kwenye sakata la Richmond na kueleza kuwa hicho ni kielelezo mojawapo cha madhara ya madaraka makubwa ya Rais Kikatiba na kusisitiza Katiba irekebishwe.

"Rais anamteua kuanzia DC hadi Jaji Mkuu. Maana yake ana nguvu dhidi ya mihimili mingine ya dola na kikatiba hawezi kuhojiwa kwa jambo lolote analofanya au maamuzi yake. Kwa Mfano maamuzi ya Bunge juu ya Richmond hayajatekelezwa yote, inaleta utata, mfano TAKUKURU inaendelea na uchunguzi wa rushwa wakati Bunge liliona kiongozi wa TAKUKURU hakueleweka kwa taarifa yake ya Richmond" alisema, Bw. Mpendazoe.

Baada ya maelezo hayo, Dkt. Hosea aliyekuwa Mwenyekiti wa Semina hiyo aliinuka na kuhoji"Unataka niteuliwe na nani? Usizungumzie haya," alisema Dkt. Hosea huku akimwamuru mbunge huyo kukaa chini.

Katika hoja yake, Bw. Mpendazoe, alisema mfumo mzima wa sasa wa Serikali umetokana na katiba ambayo ina upungufu mkubwa unaohitaji marekebisho. Alisema hata Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kuzungumzia suala hilo na kubainisha kuwa Katiba ya sasa inampa Rais madaraka makubwa yanayoweza kumfanya dikteta.

Mbunge huyo pia alikemea rushwa kwenye kura za maoni za vyama vya siasa na chaguzi za jumuiya za vyama. Alisema katika hilo, TAKUKURU inajitahidi kuchukua hatua lakini inashindwa kwasababu ni chombo cha Serikali na Serikali hiyo inatokana na chama cha siasa.

"CCM inashindwa kuchukua hatua mfano kama mhusika ni Waziri au Mjumbe wa Kamati Kuu au Halmashauri Kuu na ni kiongozi kwenye Serikali. Mapendekezo yangu nikuimarisha TAKUKURU iwe huru isiegemee chama tawala pia kuwe na Tume huru ya uchaguzi.Alisema tatizo kubwa linalochangia rushwa kuota mizizi nchini ni jamii kukumbatia jambo hilo na kutochukua hatua dhidi ya walioonekana kuhusika nayo."Albeilt Einstern alisema; Ulimwenguni pamekuwa mahali pa hatari sana kuishi lakini haitokani na uovu unaofanyika bali inatokana na wale wanaouona uovu ukitendeka na hawachukui hatua dhidi ya uovu huo."

Alisema kumekuwa na tuhuma mbalimbali zinazowakabili watu kuhusu rushwa, Serikali inapochelewa au inapokuwa haichukui hatua kwa muda mrefu, inachochea rushwa zaidi.

No comments:

Post a Comment