Sunday, May 31, 2009

Mbunge mwingine apata ajali.

Ally Sonda na Rehema Matowo, Mwanga MBUNGE wa Jimbo la Vunjo, Aloyce Kimaro amenusurika kufa baada ya gari lake alilokuwa akisafiria kuparamia mawe yaliyopangwa barabarani na kupata ajali usiku wa kuamkia jana.

Habari zinasema kuwa, ajali hiyo ilitokea katika kijiji cha Mikongeni kata ya Lembeni wilayani Mwanga, Kilimanjaro kwenye barabara kuu ya Moshi-Tanga, akiwa safarini kutoka Dar es Salaam kwenda jimboni kwake.

Kwa mujibu wa habari hizo, wakati ajali hiyo inatokea, Kimaro alikuwa na rafiki yake Joseph Temu ambaye ndiye aliyekuwa anaendesha gari hilo aina ya Mercedes Benz akiwa na mkewe na watoto wake watatu. Katika ajali hiyo hakuna aliyejeruhiwa.

Kimaro alisema baada ya ajali hiyo mfanyabiashara wa Mwanga, Shafii Hasanal alitoa msaada wa kulivuta gari hilo hadi kwenye kituo cha mafuta Kisangara.
Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Lucas Ng'oboko alisema kuwa ajali hiyo ilitokea saa 2:30 usiku, chanzo kikiwa ni mawe makubwa na matofali yaliyokuwa yamepangwa barabarani katika eneo lenye kona na mlima.

Kamanda Ng'oboko alisema kuwa watu wanaosadikiwa kuwa ni wezi, walipanga mawe hayo barabarani kwa lengo la kusababisha ajali ili kuwaibia abiria.
Gari ya mbunge huyo ilipofika katika eneo hilo likiwa katika mwendo wa kawaida na mbele yao kukiwa na lori ambalo liliweza kuyapita mawe hayo bila tatizo, wao walipojaribu kuyapita tairi la mbele upande wa kulia ya gari hilo lilipasuka wakashindwa kuendelea na safari," alisema Ng'oboko.

Kamanda huyo alisema kuwa miaka ya nyuma eneo hilo lilikuwa na matukio mengi ya aina hiyo ambayo yameanza kujitokeza upya, kwa kuwa awali wananchi wa eneo hilo kwa kushirikiana na polisi walikuwa wameyamaliza.

Alibainisha kuwa polisi wanafanya operesheni ili kuwadhibiti wezi hao na kuwasaka waliohusika na tukio hilo ili wafikishwe mbele ya sheria.
Kimaro ni miongoni mwa wabunge waliojitokeza hadharani kupambana na vitendo vya ufisadi. Mwaka jana aliibua hoja bungeni kutaka, Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa ashitakiwe kwa kutumia madaraka vibaya ya kufanya biashara akiwa ikulu.

Hii ni ajali ya pili inayohusisha wabunge kutokea ndani ya wiki mbili baada ya ajali iliyomhusisha mbunge wa Kyela, Dk Harrison Mwakyembe iliyotokea eneo la Ihemi, Ifunda mkoani Iringa.
Dk Mwakyembe, alinusurika kifo baada ya gari alilokuwa akisafiria kutoka Kyela kwenda Dar es Salaam kuacha njia na kupinduka.

Ripoti ya polisi iliyotolewa wiki hii ilieleza kwamba ajali hiyo ilitokana na uzembe wa dereva, lakini mbunge huyo ameiponda na kuifananisha na ripoti ya mpiga ramli kwa vile haikuzingatia vigezo na utaalamu katika uchunguzi .

No comments:

Post a Comment