Tuesday, May 19, 2009

waTZ waonywa kuhusu ununuaji wa magari.

Watanzania wameonywa kuwa makini na ununuzi wa magari yatokayo nchini Japan kwa kuwa kumekuwa na wimbi la magari bandia yanayoingizwa nchini kwa kutumia nembo ya nchi hiyo.

Onyo hilo limetolewa jana jijini Dar es Salaam na msafara maalumu kutoka nchini Japan uliotua nchini kwa lengo la kutoa tahadhari kwa watanzania kuwa makini na ununuzi wa magari hayo.

Msafara huo ulitoa tahadhari hiyo jana katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Willium Lukuvi.

Kiongozi wa Msafara huo kutoka nchini Japan Bw. Masahiko Imamura amesema wamekuja nchini kuonana na uongozi wa mkoa ili kutoa tahadhari kwa wananchi wa Tanzania wnaonunua magari hayo.

Amesema wamefika nchini kutokana na kupata malalamiko kutoka kwa watu mbalimbali na kudai kuwa magari ya kutoka Japan ni bandia na mabovu.

Ameongeza kuwa magari mengi yanayoletwa nchini Tanzania yamegundulika kuwa ni bandia na ambayo yanadaiwa kuwa yanatoka nchini Japan kitu ambacho si sahihi.

Amesema magari yatokayo nchini humo ni salama na uhakika kwa mtumiaji lakini wanaona kila kukicha wanapata malalamiko kutoka kwa watanzania walionunua magari hayo kusema kuwa Japan inatengeneza magari mabovu.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam amesema kuwa Watanzania wanatakiwa wachukue tahadhari kwa kuwa kuna wimbi la wafanyabiashara wanaingiza magari bandia na kudai kuwa yanatokea nchini humo.

Amesema kuwa kila kukicha jiji la Dar es Salaam kunakuwa na ongezeko la maduka ya kuuza magari na maduka mengi yanakuwa yanauza magari ambayo ni bandia si ya nchi wanazozitaja kama wanavyodai pindi unapokwenda kununua gari hizo.

No comments:

Post a Comment