Friday, June 19, 2009

ajinyakulia milioni 100 za Vodacom.

Kampuni ya simu ya mkononi ya Vodacom kupitia promosheni yake ya ‘Tuzo Milionea’ jana usiku ilimpata mshindi wa jumla wa shindano hilo Renatus Mkinga (59) ambaye alijinyakulia kiasi cha milioni 100/-
Shindano la mchezo huo lilirushwa moja kwa moja na kituo cha TBC 1.

Kupatikana kwa mshindi huyo kulifuatia mchakato mkali wa kumalizika kwa ungwe ya pili ya promosheni ya tuzo milionea ya kampuni hiyo ambayo iliwazawadia washindi 59 muda wa maongezi wa 100,000/- kutokana na droo zilizokuwa zikiendeshwa kila siku chini ya usimamizi wa bodi ya michezo ya kubahatisha.

Akizungumza na mlinda mlango anayeaminika kuwa ni nambari moja nchini, Juma Kaseja kwa njia ya simu, Mkinga mkazi wa Gongolamboto jijini Dar es Salaam ambaye ni mstaafu wa idara ya uhamiaji makao makuu alisema amefarijika baada ya kushinda nafasi hiyo.

“Kwa kweli mimi ni mstaafu wa idara ya uhamiaji ambaye maisha yangu ni kama nilikuwa najikongoja kuyaendesha, lakini kwa umilionea huu kutoka vodacom ni matarajio yangu sasa ni kukamilisha ndoto zangu kadhaa za kimaisha kama kuanzisha miradi na vitega uchumi mbalimbali,” alisema Mkinga.

Ni kama Mkinga alikuwa na bahati ya kipekee kwani kabla ya kuchaguliwa kuwa mshindi washiriki kadhaa waliotangulia licha ya namba zao kujitokeza kwenye luninga zilipopigwa hazikupatikana ama kuwa hewani jambo lililopingana na kanuni na taratibu za michezo ya kubahatisha.
“Taratibu ni kwamba anayeshiriki hana budi kupigiwa simu, apokee na kuzungumza ili kuthibitisha ushiriki wake...hivyo kwa yule asiyepokea mara tatu ama akakataa kuongea atakuwa amejikosesha ushindi,” alisema Mrisho Milao kutoka bodi ya michezo ya kubahatisha.

Akizungumzia kumalizika kwa mchakato wa kumpata mshindi wa promosheni ya pili iliyoanza Aprili, 2009, Meneja matukio na promosheni wa Vodacom, Rukia Mtingwa aliwashukuru Watanzania wote kwa waliokuwa bega kwa bega na kampuni hiyo wakati wa shindano hilo.

“Kwa niaba ya Vodacom nawashukuru wateja wetu wote walioshiriki katika promosheni hii na kwamba kumalizika kwa programu hii ni mwanzo wa mchezo mwingine utakaotangazwa baadaye,” alisema.

Mbali ya Kaseja na Milao wengine waliokuwepo kushuhudia kupatikana kwa milionea huyo wa Vodacom ni mwanariadha Dickson Marwa na Vodacom Miss Tanzania anayetarajia kukabidhi taji hivi karibuni Nasreem Karim.

No comments:

Post a Comment