Tuesday, June 9, 2009

Rais wa Gabon Afariki baada ya kutawala kwa muda wa Miaka 42.

Rais aliyekaa madarakani kwa muda mrefu zaidi kuliko marais wote barani Afrika, Omar Bongo wa Gabon amefariki dunia nchini Hispania kutokana na tatizo la moyo.
Uvumi wa kifo cha rais Omar Bongo ulizagaa tangu wiki iliyopita na kusababisha wananchi wa Gabon kuwa katika mashaka makubwa kuhusiana na hali ya usalama ya nchi hiyo.

Wananchi wengi wa Gabon walinunua chakula cha akiba na kukihifadhi majumbani mwao kwa kuhofia maduka kufungwa baada ya uvumi wa kifo cha rais Bongo kuzagaa wiki iliyopita.

Huduma ya Internet ilikatwa nchini humo tangia wiki iliyopita na televisheni ya nchi hiyo ilikuwa ikipiga nyimbo nyingi za dini.
Kifo cha rais Bongo kilithibitishwa na waziri mkuu wa Gabon Jean Eyeghe Ndong aliyetoa taarifa ya maandishi baada ya taarifa nyingi za kutatanisha juu ya kifo cha rais huyo kuzagaa.

Omar Bongo alikuwa madarakani nchini Gabon tangia mwaka 1967 na alifariki kwenye hospitali moja nchini Hispania kutokana na shambulio la moyo.
Katika taarifa yake waziri mkuu huyo alisema kwamba Gabon itatumia siku 30 kuombeleza kifo cha rais wao huyo na kuongeza “Naomba raia wote wa Gabon tushikamane pamoja katika wakati huu mgumu.”.

Hali ya mashaka imetanda nchini humo baada ya kutolewa rasmi kwa taarifa hiyo na wizara ya ulinzi ya Gabon ilitangaza kuifunga mipaka yake yote.
Wizara hiyo ya ulinzi ambayo inaongozwa na mtoto wa rais huyo aliyefariki, Ali-Ben Bongo ilitoa taarifa iliyosema kwamba majengo yote nyeti na sehemu muhimu za nchi hiyo ziko chini ya ulinzi mkali wa jeshi la nchi hiyo.

No comments:

Post a Comment