Wednesday, June 24, 2009

Wanafunzi wampiga konda,wamjeruhi.

Wanafunzi sita wa shule mbalimbali za Sekondari jijini jana waliamua kumpa kipigo konda wa gari liendalo Ubungo baada ya kuwakatalia wasiingie kwenye gari hilo.
Tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 1 kasoro za jioni katika kituo cha mabasi yaendayo Ubungo Mtaa wa Msimbazi Kariakoo jijini.
Wanafunzi hao walichoshwa na kila gari linalokuja katika kituo hicho kuwakatalia wasipande ili waweze kurejea makwao kwa kuwa muda ulizidi kusonga mbele na walichoshwa na hali hiyo.
Ndipo walipojipanga kwa pamoja na kudai kwamba gari litakalokuja sasa waweze kuonyesha msuli hadi waweze kuingia kwenye gari hilo waweze kuondoka nalo.

Gari hilo aina ya Toyota kosta ilifika kituoni hapo na kama kawaida ya makonda aliwaambia wanafunzi hao wasiingie ndani na wanafunzi hao kumwambia konda huyo lazima waondoke na gari hiyo.
Kutokana na majibu hayo ya wanafunzi hao kondakta huyo aliwaambia hakuna mtu atakayeweza kuondoka na gari hilo na atakayepanda atalipa nauli ya mtu mzima.
Wanafunzi hao ndipo walipoanza kufanya fujo kwa kushirikiana kwa pamoja kumvuta konda huyo na kumtupa chini na wao kuingia kwenye gari hilo.

Konda huyo hakuridhika na alitoa amri kwa dereva kuwa asiondoe gari hadi wanafunzi hao washuke chini na wanafunzi hao waliendelea kugoma kushuka chini na baadhi ya abiria kuwatetea.
Konda huyo alianza kumkunja shati mmoja wa wanafunzi hao na kuanza kumpiga ndipo wote kwa pamoja walijiunga kumshambulia konda huyo na kumjeruhi vibaya.

Kuona hivyo dereva aliamua kuondoa gari kwa kuwa aliona hata akienda kituo cha polisi sheria itambana konda wake kwa kuchukua uamuzi wa kumpiga mwanafunzi.

Konda huyo alijeruhiwa sehemu za uso na sehemu zingine za mwili na wanafunzi hao kufaulu kuondoka na gari hilo.

Tatizo la usafiri hasa kwa upande wa wanafunzi limekuwa ni kubwa na imekuwa ni kero kwa wanafunzi na hata watu wazima katika jiji la dar es salaam na hata kwingineko mikoani pia, hivyo mtandao huu unachukua fursa hii kuiomba serikali kulifuatilia kwa ukaribu hususani suala zima la unyanyasaji wa wanafunzi kwenye madaladala.

No comments:

Post a Comment