Thursday, June 11, 2009

Zitto Kabwe atangaza kung’atuka.


MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, ametangaza kung’atuka katika wadhifa wake mwaka 2010.
Kabwe alitangaza adhima yake hiyo jana, wakati akiongea na waandishi wa habari katika Hoteli ya Greenbeach mjini Maswa mkoani Shinyanga.
Alisema amefikia uamuzi huo bila kushinikizwa na mtu yeyote na ameamua kutangaza mapema ili kutoa nafasi kwa wanaotaka kugombea nafasi hiyo, ili wajiandae.
Kabwe alisema anatamani kufanya kazi za kitaalamu, hasa zinazohusu taaluma yake baada ya kuwa mwakilishi wa wananchi kwa kipindi cha miaka mitano.
“Tangu nimalize masomo yangu chuo kikuu, ni kipindi cha mwaka mmoja tu niliofanya kazi kisha nikachaguliwa kuwa mbunge, hivyo nina hamu ya kufanya kazi nyingine mbali na hii ya uwakilishi,” alisema Kabwe.
Alisema uamuzi wake wa kuachana na ubunge hauhusuni na masuala ya siasa ambayo iko katika damu yake.
Kabwe alisema kamwe hataachana na siasa bali baada ya kuachana na ubunge, ataendelea kufanya kazi za kuiimarisha CHADEMA ambayo imemfikisha katika mafanikio aliyonayo sasa.
Aliahidi kuendelea kuwatumikia wananchi wa Jimbo la Kigoma Kaskazini kwa uaminifu na kushirikiana nao kuondoa kero mbalimbali zinazowakabiri pamoja na kutimiza ahadi zake alizozitoa wakati wa kuomba kura.
Kabwe alionya kuwa kazi ya ubunge si lelemama kama baadhi ya watu wanavyofikiria, bali ni ngumu na inayohitaji uvumilivu wa hali ya juu.
“Nimeifanya kazi hii ya ubunge kwa muda wa mwaka mmoja sasa, si kazi ya lelemama, ni lazima ujitolee kweli kuwatumikia watu, kwani kila tatizo linapotokea jimboni wananchi wanakutazama wewe mbunge,” alisema Kabwe.
Kabwe ni miongoni mwa wabunge vijana wa CHADEMA ambaye katika Uchaguzi Mkuu wa vyama vingi wa mwaka 2005 alifanikiwa kuwashinda wagombea wa vyama vingine vya siasa.

No comments:

Post a Comment