Friday, June 12, 2009

aliyenusurika kwenye ajali ya ndege,afa kwa ajali ya gari.

Mwanamke wa Italia ambaye alinusurika kufariki kwenye ajali ya ndege ya Ufaransa iliyodondoka kwenye bahari ya Atlantic baada ya kuchelewa uwanja wa ndege amefariki siku chache baadae kwa ajali ya gari.

Johanna Ganthaler na mumewe Kurt walikuwa kwenye vakesheni nchini Brazili na walikuwa wanatakiwa wapande ndege ya Ufaransa namba 447 kuelekea Paris lakini kwa bahati nzuri waliikosa ndege hiyo baada ya kuchelewa uwanja wa ndege.
Johanna na mumewe walipanda ndege nyingine baada ya kuikosa ndege hiyo ya Ufaransa.

Watu wote 228 waliokuwemo kwenye ndege ya Ufaransa walifariki dunia baada ya ndege hiyo kuangukia kwenye bahari ya Atlantic.
Wataalamu wa masuala ya ndege bado wanaendelea kutafuta chanzo halisi kilichosababisha kuanguka kwa ndege hiyo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Italia, ANSA, gari waliyokuwemo Johanna na mumewe ilitoka kwenye njia yake barabarani na kulivaa lori lililokuwa linakuja upande wa pili.

Katika ajali hiyo iliyotokea nchini Austria, Johanna alifariki hapo hapo wakati mumewe alipata majeraha makubwa.
Johanna alikuwa ni mkazi wa kitongoji cha Bolzano-Bozen nchini Italia.

Wakati huo huo jumla ya maiti 44 kati ya 228 za abiria waliokuwemo kwenye ndege ya Ufaransa zimepatikana hadi sasa kwenye bahari ya Atlantic.

Zoezi la kutafuta maiti zaidi za abiria waliokuwemo kwenye ndege hiyo linaendelea ingawa zoezi hilo limepangwa kusitishwa wiki ijayo.

No comments:

Post a Comment