Saturday, June 13, 2009

Uwanja Mpya wa Taifa Kutumiwa na Timu zitakazoshiriki Kombe la Dunia.

Uwanja mpya wa taifa huenda ukatumiwa na timu zitakazoshiriki kombe la dunia mwakani nchini Afrika Kusini kama mipango iliyopangwa itafanikiwa.

Katika kuutangaza uwanja mpya wa taifa, Naibu Waziri wa Michezo na Utamaduni, Mh. Joel Bendera alisema kuwa kuna kamati imeundwa ili kuutangaza uwanja mpya wa taifa katika kipindi cha mashindano ya kombe la dunia yatakofanyika mwakani nchini Afrika Kusini.

Kamati hiyo tayari ipo kwenye mipango thabiti ya kuhakikisha uwanja mpya wa taifa unatangazwa hasa kwa kupitia mashindano hayo kwa kuzipa nafasi timu zitakazoshiriki mashindano hayo kutoka mabara yote duniani kuja kufanya mazoezi yao nchini kabla hazijaelekea Afrika Kusini.

Akiongea jana wakati wa mapumziko ya Bunge, Mh. Bendera alisema kuwa kutokana na sheria za FIFA ambazo zinaitaka timu iwe imeishafika nchini Afrika Kusini siku saba kabla ya mechi yake, huenda ikawa vigumu kwa timu kuja kuweka kambi hapa nchini lakini ni rahisi kwa washabiki wake kuweka kambi nchini kwani kutoka Tanzania hadi Afrika Kusini ni masaa manne kwa ndege.

Mh. Bendera alisema kuwa wizara ya michezo ipo katika maandalizi makubwa kuhakikisha wadau wengine wanashirikishwa katika zoezi hilo la kuutangaza uwanja mpya wa taifa ambao ni miongoni mwa viwanja vya hadhi ya juu sana barani Afrika.

Kamati iliyoundwa itafanya mawasiliano na shirikisho la soka la Afrika Kusini ili kujua ni namna gani wanaweza wakafanikisha zoezi hilo.

No comments:

Post a Comment