Saturday, June 13, 2009

watoto wajiuza kwa malipo ya chakula-zimbabwe.


Hali ngumu ya uchumi nchini Zimbabwe imepelekea watoto wengi nchini humo wenye umri kuanzia miaka 12 kujiingiza kwenye ukahaba wakifanya mapenzi kwa malipo ya chakula au kitu chochote ambacho mtu anaweza kutoa.
Shirika la hisani la kuwasaidia watoto nchini Zimbabwe la Save the Children lilisema kwamba hali ya ufukara ambayo imezidi kuzikumba familia nyingi nchini humo imesababisha watoto wengi wa kike kuingia kwenye ukahaba ili wawape pesa za kuganga njaa.
Shirika hilo lilisema kuwa watoto wenye umri kuanzia miaka 12 wanaiuza miili yao kwa chakula au vitu vidogo vidogo vya kuganga njaa kama vile biskuti.
Shirika hilo lilidai pia kwamba kombe la dunia ambalo litaanza nchi jirani ya Afrika Kusini mwakani litafanya hali iwe mbaya zaidi nchini Zimbabwe.
Idadi ya watu ambao hawana kazi nchini Zimbabwe inakadiriwa kufikia asilimia 90 ya watu wote na wengi wao hawana uwezo wa kujinunulia chakula, madawa au kulipa ada za shule.
Mwalimu mkuu msaidizi wa shule moja nchini humo yenye wanafunzi 1,500 aliliambia shirika la habari la Uingereza BBC kwamba mamia ya wanafunzi wake wa kike wanaiuza miili yao kwa kitu chochote wanachoweza kupata.
"Wanaweza wakapewa vitabu, au biskuti au chipsi yani chochote ambacho mtu anaweza kutoa".
Mwanafunzi mmoja wa shule hiyo mwenye umri wa miaka 14 ambaye hakutaka kutaja jina lake alisema kuwa anawajua wasichana wengi wenye umri mdogo ambao hivi sasa wamekuwa makahaba.

Yeye mwenyewe alisema kuwa yuko kwenye njia panda ya kujiunga nao kwani maisha yake yamekuwa magumu sana baada ya kufariki kwa wazazi wake wote wawili.

No comments:

Post a Comment