Thursday, July 16, 2009

Jitihada za Kutafuta Urembo wa Ziada zamgharimu

Jitihada za kutafuta urembo wa ziada za mwanamke mmoja wa nchini Marekani zilimtokea puani baada ya sura yake kuharibika vibaya kiasi cha kuwa vigumu kutambulika alipoamua kujidunga sindano za urembo za silikoni.
Mary Johnson mwenye umri wa miaka 54 mkazi wa California nchini Marekani katika jitihada zake za kutafuta urembo wa ziada aliamua kufanya upasuaji wa kurekebisha sura yake aonekane kijana na mrembo.
Lakini Mary ambaye ni mama wa watoto watatu alipoambiwa kuwa upasuaji wa kurekebisha sura yake utamgharimu maelfu ya dola za Marekani, aliamua kughairi kufanya upasuaji huo hospitalini na kuamua kutumia njia za kujidunga sindano za silikoni.
Baada ya kufanya utafiti kwenye Internet Mary alinunua sindano za kimiminika cha silikoni kwa dola 10 tu na kujidunga mwenyewe kwenye mdomo wake na kwenye mashavu yake.
Badala ya sindano hizo kumfanya aonekane mrembo kama alivyotarajia, ziliiharibu kabisa sura yake na kuifanya iwe vigumu kwa mtu kumtambua.
Baada ya muda mfupi sura yake ilianza kubadilika rangi na kuvimba na kwenye kona za mdomo wake kulitokea vidonda vikubwa visivyoeleweka.
Hali ilikuwa mbaya kiasi cha kusababisha Mary awahishwe hospitali na kufanyiwa upasuaji wa kuifanya sura yake irudie hali yake ya zamani.

Hivi sasa ingawa sura ya Mary imerudia hali yake ya zamani, Mary anakiri kujutia uamuzi wake wa kutafuta urembo wa ziada.

No comments:

Post a Comment