Wednesday, July 8, 2009

Mrisho Mpoto anusurika kwenye ajali.

Mrisho Mpoto ‘Mjomba’, Jumamosi iliyopita ameripotiwa kunusurika katika ajali ya gari iliyotokea katika kijiji cha Mnonela, Lindi Vijijini majira ya saa 7: 25 mchana.
Mpoto alikuwa akiendesha gari aina ya Mark 11 gx 100 Saloon yenye namba T424 AQR, mali ya mfanyabiashara maarufu wa mjini Mtwara, Abdul Swamadu, alipata ajali katika eneo hilo linalofanyiwa ukarabati.
Akiwa katika mwendo wa kasi, Mjomba ghafla aliona magogo yamepangwa barabarani huku upande wa kulia kwake kukiwa na kona, hivyo akaingia barabara ndogo ambayo pia inakarabatiwa.
Kwa mujibu wa habari zilizopatikana na kusambazwa katika vyombo vya habari, Mjomba alisema baada ya kukunja kona, gari lilimshinda na kuyapanda magogo yaliyopangwa barabarani, hivyo gari kurukia upande wa pili na kusimama.

Hata hivyo, Mjomba’ alisema anashumkuru Mungu kwani yeye na wenzake waliokuwamo katika gari hiyo, walitoka salama isipokuwa gari imeharibika vibaya sehemu ya mbele huku rejeta ikipasuka.
Alisema, baada ya ajali hiyo, walirejea Mtwara na kumwarifu mmiliki wa gari ambaye alikwenda kulivuta hadi gereji kwa ajili ya matengenezo.

Chanzo cha ajali hiyo kinatokana na kukosekana kwa alama ya kuonyesha kama mbele kuna matengenezo ya barabara au kona ili kuepusha matukio kama hayo.
Mjomba, alienda Mtwara kwenye maadhimisho ya siku ya ushirika duniani ambayo kilele chake kilikuwa Julai 4.
Mbali ya Mjomba, wasanii wengine walioshiriki ni Halila Tongolanga na Makondeko Musica ambao kwa nyakati tofauti, walifanya vitu vyao.

No comments:

Post a Comment