Thursday, July 9, 2009

Wamiliki wa kampuni iliyochota EPA watajwa mahakamani

Msajili Msaidizi wa Wakala wa Usajili wa Kampuni (Brela), Noel Shai amewataja katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, Paul Nyingo na Fundi Kitunga kuwa ni wamiliki wa kampuni ya Monney Planers & Consultants.

Aliyataja majina hayo jana mbele ya jopo la mahakimu watatu, Benedict Muingwa, Catherine Revocate na Fatma Masengi wakati alipokuwa akitoa ushahidi katika kesi ya wizi wa fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) zilizotunzwa Benki Kuu ya Tanzania inayomkabili kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rajabu Maranda na Farijala Hussein.

Shai alidai anaifahamu kampuni hiyo ya Monney Planers & Consultants kama ni moja ya jina la biashara lililowahi kusajiliwa na Brela na kwamba hati zake za usajili alizisaini yeye mwenyewe.
Alidai alizisaini nyaraka hizo kwa sababu zilikuwa ndani ya majukumu yake ambayo ni kupitia, kukubali au kukataa maombi ya usajili wa majina ya biashara na makampuni pamoja na kusaini vyeti.
Aliendelea kudai kwamba, Machi 22, 2005 yalifanyika maombi ya kuisajili kampuni hiyo ya Monney Planers & Consultants ambayo ilipewa namba ya usajili 150731 kwa jina la Nyingo na Kitunga ambao pia ndio walioruhusiwa kuendesha akaunti za benki katika kampuni hiyo.


Alidai Machi 23, 2005 maombi ya usajili wa kampuni hiyo yalikubaliwa na kupitishwa na Msajili Msaidizi wa Brela, Rehema Kitambi na kwamba Machi 24, 2005 yeye alizisaini nyaraka hizo za usajili. Aliongeza kuwa sheria ya biashara inakataza mtu kusajili majina zaidi ya mawili yanayofanana.
Hata hivyo Shai aliongeza kudai kuwa hakuna mabadiliko yoyote yaliyowahi kufanyika katika kampuni hiyo tangu Machi 22, 2005 iliposajiliwa hadi sasa.


Farijara na Shabani wanadaiwa kuwa kati ya Machi 22 na Desemba 7, 2005 jijini Dar es Salaam, waligushi nyaraka mbalimbali na kuiibia BoT Sh 2,266,049,041.25 kupitia kampuni yao ya Monney Planers & Consultants baada ya kudaganya kuwa ilipewa deni na kampuni ya B. Grancel & Co ya nchini Ujerumani.

No comments:

Post a Comment