Friday, July 10, 2009

mafua ya nguruwe yaingia nchini.

Serikali imetoa tahadhari kwa wananchi kuwa makini kuhusu ugonjwa wa mafua ya nguruwe baada raia wa Uingereza aliyeingia nchini mwishoni mwa wiki kugundulika kuwa na ugonjwa huo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Aisha Kigoda alisema wananchi wanatakiwa kuwa makini na ugonjwa huo na kutoa taarifa mara wanapoona mtu mwenye dalili zake.


“Mgonjwa huyo aligundulika nchini Julai 4 mwaka huu baada ya kuwasili nchini akitokea London, Uingereza kwa kutumia ndege ya Kenya ambayo ilipitia Nairobi kabla ya kuwasili nchini,” alisema Dk Kigoda.

Alitaja dalili za ugonjwa huo Dk Kigoda kuwa ni homa ya ghafla, kuumwa kichwa, maumivu ya viungo, maumivu ya misuli na uchovu wa mwili.
Alisema dalili nyingine ni pamoja na kikohozi, mafua, maumivu ya koo, kichefuchefu, kusikia dalili za mwili kutetemeka na kukosa hamu ya kula.


Aliongeza kuwa wakati mwingine mgonjwa anaweza kuharisha na kutapika na kwamba wagonjwa wengine huzidiwa na kupata vichomi pamoja na kushindwa kupumua.
Kuhusu namna ambavyo mgonjwa huyo anaweza kuzuilika kwa kuchukua tahadhari, Waziri Kigoda alisema: “Mgonjwa anaweza kuziba mdomo na pua kwa kitambaa au kwa karatasi laini wakati anapokohoa ama kupiga chafya.


Dk Kigoda alisema kuwa mgonjwa huyo aliyegundulika ni mwanafunzi aliingia nchini kupitia uwanja wa kimataifa wa ndege wa Julius Nyerere.
Dk Kigoda alisema mgonjwa huyo aliwasili akiwa pamoja na wenzake 15 na walimu wanne kwa ajili ya mafunzo na kupanda milima wakati wa likizo yao ya majira ya joto.


“Mgonjwa huyo aligundulika mara alipowasili uwanja wa ndege baada ya kujaza fomu maalum ambazo hujazwa na abiria wote wanaowasili uwanjani hapo kutoka nje ya nchi,” alisema Kigoda.
Waziri Kigoda aliongeza kuwa baada ya kujaza fomu hizo mgonjwa huyo aligundulika kuwa na dalili za ugonjwa wa mafua ya nguruwe na wataalamu walimchukua na kumpeleka chumba maalumu kwa ajili ya kuchukua vipimo ambavyo vilionyesha kuwa ana ugonjwa huo.


Kigoda alisema vipimo hivyo vilipelekwa katika maabara ya Taasisi ya Uchunguzi wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) na vingine kwenye maabara ya Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO Reference Labaratory) iliyopo Kemri, Nairobi nchini Kenya na matokeo yote kuthibitisha kuwa ana ugonjwa huo.

Dk Kigoda alisema mgonjwa huyo alipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kwa sasa amelazwa katika wodi maalum ya magonjwa ya kuambukiza na anaendelea vizuri na dalili zote za ugonjwa zimetoweka na ataendelea kuwepo hospitalini hapo mpaka atakapomaliza matibabu yake.

Waziri Kigoda alisema hata hivyo uchunguzi uliofanywa kwa wanafunzi waliobaki pamoja na walimu wao umebaini kuwa hakuna yeyote aliyeonekana kuwa na dalili za ugonjwa huo.
Hata hivyo wizara hiyo imeshasambaza dawa 50,000 kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) ili kukabiliana na tatizo hilo na kuimarisha wodi maalum za wagonjwa na kutoa elimu ya afya kwa wafanyakazi na wananchi.


Alisema ugonjwa huo unazuilika endapo wananchi watafuata sheria za afya kama vile kunawa mikono vizuri kwa sabuni mara kwa mara na kuepuka kuwa karibu na mtu ambaye ana dalili za ugonjwa huo wa mafua ya nguruwe, pamoja na kuzuia mdomo na pua kwa kitambaa au karatasi laini wakati wa kukohoa au kupiga chafya na kuepuka kula au kuchinja nguruwe ambaye anaonyesha dalili za ugonjwa huo.

Kwa mara ya kwanza ugonjwa huo uligundulika nchini Mexico ambapo watu kadhaa waliripotiwa kufa na wengine kupata maambukizo.
Baadaye ugonjwa huo ulienea katika nchi mbalimbli duniani na katika nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara ulioripotiwa kuingia katika nchi za Afrika ya Kusini na Misri.


Katika kanda ya Afrika ya Mashariki na Kati, ugonjwa huo uliripotiwa kwa mara ya kwanza nchini Kenya ambako mwanafunzi mmoja raia wa Uingereza alibainika kuwa na ugonjwa huo wakati akiingia na kwa sasa kuna wagonjwa 15 na wengine 30 wanasubiri matokeo ya uchunguzi wa afya zao.

No comments:

Post a Comment