Friday, July 31, 2009

nmb temeke yavamiwa na majambazi.

Mtu mmoja amefariki na wengine 13 kujeruhiwa wakati majambazi ambayo idadi yao haikujulikana mara moja huku yakiwa na silaha nzito pamoja na mabomu yalipovamia na kupora mamilioni ya shilingi katika tawi la benki ya NMB Temeke.

Majambazi hayo ambayo idadi yao haikujulikana mapema wakiwa na silaha nzito na pamoja mabomu ya mkono yalivamia tawi la benki ya NMB lililopo Temeke na kupora pesa zinazokadiriwa kufikia TSh. Milioni 150.
Katika purukushani hiyo iliyotokea leo asubuhi, majambazi hayo yalimuua mlinzi wa benki hiyo na kujeruhi watu wengine 13 ndani ya tawi la benki hiyo.

Taarifa zinasema kwamba majambazi hayo yalipofika eneo la benki hiyo yalirusha mabomu mawili ya mikono yaliyosababisha kifo cha mlinzi wa benki hiyo na ndipo yalipoanza kupiga risasi hovyo katika harakati zao za kupora pesa kwenye benki hiyo.
Baada ya kufanya uhalifu huo majambazi hayo yalitoroka na kutokomea yakiwa katika magari mawili yenye namba zinazoanzia na "STJ" na "SU".

Viongozi wa serikali wakiongozwa na waziri wa mambo ya ndani Mh. Lawrence Masha, mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai Robert Manumba, mkuu wa Polisi IGP Saidi Mwema na mkuu wa mkoa wa Dar Mh. William Lukuvi walitembelea eneo la tukio na kisha kuwatembelea wagonjwa waliokuwa wamelazwa katika hospitali ya Temeke.
Msako mkali umeanzishwa na jeshi la polisi kuwasaka na kuwabaini majambazi hayo.

No comments:

Post a Comment