Monday, July 6, 2009

Uchunguzi wa Karamagi, Msabaha wazua mambo mengi.

Ikiwa sasa ni miaka takriban miwili tangu serikali itangaze kufanya uchunguzi dhidi ya mawaziri wawili wa zamani, Dk Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi, kuhusika katika kashfa ya utoaji zabuni ya kufua umeme wa dharura kwa kampuni ya Richmond Development (LLC), suala hilo linaonekana kugubikwa na giza.
Septemba mwaka jana, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema kuwa serikali inachunguza kama mawaziri hao wawili walihusika kwenye vitendo vya rushwa wakati wa zabuni kwa kampuni hiyo ya Richmond licha ya uamuzi wao wa kujiuzulu, sambamba na waziri mkuu wa wakati huo, Edward Lowasa, baada ya kutajwa kwenye kashfa hiyo.


Wakati Richmond ikipewa mkataba huo, Msabaha alikuwa Waziri wa Nishati na Madini lakini akaondolewa kwenye mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri na nafasi yake kuchukuliwa na Karamagi, ambaye alisimamia wakati mkataba wa Richmond ukirithishwa kwa kampuni ya Dowans Tanzania Limited.

Serikali iliamua kuwachunguza mawaziri hao baada ya Bunge kupitisha maazimio 23 ya kushughulikia kashfa hiyo baada ya ripoti ya uchunguzi wa kamati teule iliyokuwa chini ya Dk Harrison Mwakyembe iliyowasilishwa kwenye mkutano wa 10 wa bunge, mwezi Februari mwaka 2008 na Lowassa kuachia uwaziri mkuu na baadaye kufuatiwa na Karamagi na Msabaha.
Hata hivyo, tangu mkutano huo wa kumi hadi wakati huu ambao Bunge linaendelea na mkutano wa 16, matokeo ya uchunguzi dhidi ya mawaziri hao bado hayajawekwa bayana, wakati watendaji ambao mkutano huo ulitaka wachukuliwe hatua na mamlaka husika, bado wanaendelea na majukumu yao.


Wakati serikali ikishindwa kutoa tamko bungeni, watendaji wa vyombo vya dola vinavyohusika na uchunguzi na mashitaka, nao wamekuwa wakipiga danadana kuzungumzia sakata hilo.

Alipoulizwa kuhusu suala hilo wiki iliyopita, Mkurugenzi wa Mashitika (DDP), Eliezer Feleshi aliagiza akatafutwe msaidizi wake.

"Hebu mtafute msaidizi wangu ofisini maana yeye ndiye nimemwachia ofisi. Kwa sasa niko nje ya ofisi hivyo siwezi kuwa na taarifa sahihi za majalada hayo," alisema DPP Feleshi mwanzoni mwa wiki iliyopita.

Hata alipoulizwa sababu za ofisi yake kutotoa taarifa zozote licha ya kufanyiwa kazi kwa muda mrefu, alijibu: "Nisikilize bwana (alitaja jina la mwandishi), nenda ofisini."
Lakini alipofuatwa msaidizi huyo, alisema mkuu wake (Feleshi) hakuwa amemwachia majalada hayo mezani kwake wala hayajamfikia na alipoelezwa kwamba Feleshi ndio ameagiza atoe taarifa hizo, alijibu: "Unaweza kukasimiwa madaraka, lakini si kila kitu unaweza kupewa au kukifanya."
Naye Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba amekuwa akieleza kwa wiki nzima kuwa hajapata taarifa zozote kutoka jopo lake la uchunguzi.


"Sijapata taarifa... nafikiri subiri nitafute jopo la uchunguzi ndipo nikupe jibu," alisema Manumba Jumatatu iliyopita akirejea jibu ambalo amekuwa akilitoa kila mara anapoulizwa kuhusu suala hilo.

Katika mkutano huo wa 10 wa bunge, sakata la Richmond lilitikisa nchi baada ya kubainika kuwa serikali ilitoa zabuni kwa kampuni hiyo wakati ilikuwa haikidhi vigezo mbalimbali na kwamba kulikuwa na dalili za rushwa. Mkataba huo ulisainiwa muda mfupi baada ya serikali ya awamu ya nne kuingia madarakani na kukumbana na tatizo kubwa la ukame.

Kufichuliwa kwa uzandiki kwenye suala hilo na kujiuzulu kwa Lowassa, kulisababisha Rais Kikwete avunje Baraza la Mawaziri.

Bunge kwa pamoja liliridhia na kupitisha maazimio 23 na kati ya hayo saba yalitokana na michango ya wabunge na Bunge lilitoa miezi mitatu kwa serikali kuyatekeleza na kutoa taarifa. Hata hivyo, utekelezaji huo umekuwa ukienda taratibu.

Miongoni mwa maazimio hayo ni azimio namba nane na 14 ambayo yalitaka maziri wanaohusika na nishati na madini kwa nyakati tofauti wakati wa mkataba huo na urithishwaji wake, wawajibishwe na katika taarifa ya utekelezaji mawaziri hao walikuwa wameshajiuzulu hata kabla ya kuwajibishwa na rais.

Maazimio mengine yalimuhusu mwanasheria mkuu, Johnson Mwanyika aliyetakiwa awajibishwe na rais kutokana na kushindwa kuwajibika hadi wasaidizi wake wakafanya taifa likaingia hasara, lakini taarifa ya utekelezaji ilieleza kuwa aliandikiwa barua kumtaka aeleze sababu za kutowajibika. Chenge alijiuzulu mapema mwaka huu baada ya kuhusishwa kwenye kashfa ya ununuzi wa rada.

Pia azimio jingine (namba tisa), lilitaka mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ambaye ni Edward Hosea awajibishwe na rais baada ya taasisi yake kutoa taarifa iliyoisafisha Richmond, lakini ilielezwa kuwa Hosea alishajitetea kwa katibu mkuu kiongozi.

No comments:

Post a Comment