Monday, September 7, 2009

Vyama vyaunga mkono uandikishaji kuanza tena

Vyama vya siasa kisiwani Pemba vimeunga mkono uamuzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar(ZEC) kuanza tena kazi ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura katika miko ya Kaskazini Pemba na Kaskazini Unguja baada ya kusitishwa kwa kazi hiyo mwezi uliopita.

Vyama vilivyounga mkono uamuzi huo ni pamoja na CCM, Chadema, Muungano wa Wakulima Tanzania (AFP) na National League for Deomcracy(NLD).
Katibu wa Chadema mkoani Kusini Pemba, Mohammed Ali Salim alisema kwamba chama chake kimeridhishwa na hatua ya Zec kutangaza kuanza tena kwa uandikishaji wapigakura hasa ikizingatiwa kuwa wananchi wengi wanaendelea kupata vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi (Zan ID) baada ya kuwekwa kwa utaratibu wa shehia mbili mbili kusajili wakaazi.


"Umefika wakati sasa Tume ya Uchaguzi ijiamini katika maamuzi yake inayoyatoa baada ya kujiridhisha na sio kuburuzwa na vyama vya siasa vya CCM na CUF wakati suala la uchaguzi linahusiaha wananchi wote," alisema kiongozi huyo wa Chadema.
Mwenyekiti wa AFP, Said Soud Said alivitaka vyama vya siasa kuachana na mambo yenye kulenga kuvuruga demokrasia kwa kuwa mambo ya uchaguzi ni wa watu wote bila kuzingatia itikadi za siasa.
Alisema kuendelea kung'ang'ania kusitishwa kwa uandikishaji kunaweza kusababisha athari kubwa na kuvuruga ratiba ya Zec ya uandikishaji na mchakato mzima wa uchaguzi mkuu, hali ambaye alisema inaweza kumfanya rais aliye madarakani kuendelea kutawala kwa kuwa hakutakuwa na uchaguzi.


"Tume inapaswa kuelewa kwamba imepanga ratiba yake ambayo ni lazima iifuate na kwa kuwa wanafanya kazi kwa mujibu wa sheria, hatutegemei tena kufanya maamuzi kwa shinikizo la vyama vya siasa kama walivyofanya awali," alitahadharisha mwenyekiti huyo wa AFP.
Katibu wa CCM wilayani Chake Chake, Zainab Khamis Shomari alisema chama chake kinaunga mkono uamuzi huo tangu awali kwani walitumia muda mwingi kuwaelimisha wanachama na wafuasi wake wakati wa zoezi la usajili wa vitambulisho mwaka 2005, hivyo hawana shaka yoyote.


Alisema kwamba Zec ilikuwa ikikiuka sheria na katiba za nchi kwa kusitisha uandikishaji bila kuwa na sababu za msingi na hasa ikizingatiwa kuwa wengi wa wananchi kisiwani Pemba walikuwa wanajitokeza kwa ajili ya kujiandikishaji katika daftari la kudumu.
Naibu katibu mkuu wa NLD, Rashid Ahmed Rashid alisema chama chake kimefanya ziara katika mikoa miwili ya Pemba na wilaya zake na kujiridhisha kwamba kazi ya uendelezaji wa daftari la kudumu la wapigakura inaweza kufanyika, tena kwa ufanisi mkubwa.
Rashid alisema kwam ba tangu Idara ya Usajili wa Vitambulisho ianzishe mfumo mpya wa kusajili watu katika shehia zao kwa kutoa siku mbili kwa kila shehia, kumekuwa na mafanikio makubwa kwa watu kupata vitambulisho hivyo.

Katibu wa CUF wilayani Chake Chake, Saleh Nassor alisema hawaungi mkono kuanza tena kwa zoezi hilo kwa madai kuwa kuna watu wengi hawanajapata vitambulisho.
Tume ya Uchaguzi Zanzibar ilisitisha uandikishaji wapigakura katika daftari la kudumu katika mkoa wa Kaskazini Pemba baada ya kutokea kwa vurugu Wete mwezi uliopita.

No comments:

Post a Comment