Wednesday, September 2, 2009

Watanzania Wawili Wafariki Wakizamia Meli sauzi

Watanzania wawili kati ya wanne waliozamia meli ya mizigo iliyokuwa ikielekea Afrika Kusini wamefariki ndani ya meli hiyo baada ya kujificha ndani ya meli hiyo kwa siku tisa.

Miili ya watanzania wawili kati ya wanne waliozamia meli kwa nia ya kuingia nchini Afrika Kusini, iliopolewa kutoka kwenye meli ya makontena wakati ilipotia nanga Durban nchini Afrika Kusini.
Watanzania hao wanne ambao wote walikuwa ni ndugu walizamia kwenye meli hiyo ya mizigo na kujificha ndani ya meli hiyo kwa siku tisa hadi siku walipogundulika.

Wakati wawili wakifariki ndani ya meli hiyo, wawili wanaendelea na matibabu kwenye hospitali ya Life Entabeni Hospital ya mjini Durban.
Watanzania hao ndugu waligundulika baada ya wafanyakazi wa meli hiyo kusikia kelele zikitokea kwenye vyumba vya injini ya meli hiyo.
Polisi wa Afrika Kusini walisema kwamba, vijana hao baada ya kuokolewa waliwaambia polisi kuwa binamu zao walipotea kwenye meli hiyo wakati bahari ilipochafuka na kuwa na kuwa na upepo mkali siku moja kabla hawajaokolewa.

Miili ya ndugu hao waliofariki ilikutwa kwenye chumba cha mapangaboi ya usukani wa meli hiyo.Awali vijana hao walipookolewa waliwaambia polisi kuwa wao ni raia wa Ghana lakini baadae walianza kubadilisha kauli na kutaja nchi tofauti tofauti.
Baadae polisi walithibitisha kuwa vijana hao ni watanzania.
Taarifa zilisema kwamba polisi wa Afrika Kusini wana mpango wa kufukuza nchini humo vijana hao wa kitanzania bila ya kuwafikisha mahakamani kwa kuingia nchini humo kinyume cha sheria lakini kama kutakuwa na utata katika vifo vya ndugu zao watafikishwa mahakamani kwanza kabla ya kurudishwa bongo.

Taarifa zaidi zilisema kwamba ubalozi wa Tanzania nchini humo umeishataarifiwa suala hilo na taratibu za kuwakabidhi miili ya vijana wawili waliofariki zinafanywa na polisi wa kimataifa interpol.

No comments:

Post a Comment