Tuesday, September 1, 2009

Walimu waliopigwa viboko kudai fidia kortini

Walimu waliochapwa viboko na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Vijijini, Albert Mnali, wamepanga kufungua kesi katika Mahakama Kuu ya Tanzania, kudai fidia na kutafuta haki ya kisheria.
Febuari mwaka huu, Mnali aliwacharaza viboko zaidi ya walimu 30 wa shule tatu za msingi za Bukoba Vijijini, kufuatia halmashauri hiyo kuwa ya mwisho, kimkoa katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba, matokeo ambayo alisema yalitokana na uzembe wa walimu hao.
Mmoja wa walimu hao, Avitus Leornad wa Shule ya Msingi Katerero alisema kuwa maandalizi ya kufungua kesi hiyo yamekamilika.
“Tumeshampata wakili na muda wowote tutaifungua kesi hiyo Mahakama Kuu ya Tanzania, kudai fidia ya kudhalilishwa,” alisema Avitus.
Alipoulizwa kwamba hawaoni wamechelewa kufungua kesi hiyo hasa baada ya mlengwa (DC) kufukuzwa kazi, alisema “ni kweli Mnali alifukuzwa kazi lakini ikumbukwe kuwa alitudhalilisha akiwa mtumishi wa serikali ambayo bado iko madarakani.
Siku chache baada ya mkuu huyo wa wilaya kuwacharaza viboko walimu hao, Rais Jakaya Kikwete alimfukuza kazi ingawa mwenyewe (Mnali) aliendelea kusisitiza kuwa pamoja na uamuzi huo, ujumbe umefika.
Mbali na Avitus Leornad, walimu wengine waliochapwa viboko na Mnali ni Generosa Lwakatare, Ernestina Anatory, Jonesta Grenos, Hawa Ayubu, Rehema Baisi, Frieda Laurian, Avitus Leornad na Asirath Ndyamukama wa Shule ya Msingi Katerero.
Wengine ni Amosi Kamugisha, JK Zale, Bruno Francis, Mwesiga, Pulleti Rugemalila, Winfrida Kakurwa, Editha Bigilwa, Ester Mutashaba, Ludovic Bushongole, Gosbert William,Venance Philipo na edasto Munabi, wa Shule ya Msingi Kasenene.
Wengine Imelda Lwegalulila, Coretha Ernest, Devotha Bushobe, Augustina Bampenja, Josephina Ndyamukama, Julius Katemana, Videlieth Yesse, Generoza Mulokozi, Syvester Petro, Josiah Kamuhabwa na Concessa Rweyemamu wa Shule ya Msingi Kanazi.

No comments:

Post a Comment