Monday, August 31, 2009

Chuo Kikuu Huria chabadili mfumo wa kufanya mitihani

Chuo kikuu Huria Tanzania kimebadili mfumo wa utoaji majaribio kutoka mara tano kwa mwaka hadi mara mbili, ili kuongeza ufanisi na ubora wa kukuza uwezo wa wanafunzi katika kufaulu mitihani.
Akizungumza katika mkutano wa Wahadhiri na wanafunzi wa chuo hicho, Makamu Mkuu wa chuo Tolly Mbwette, alisema mfumo huo mpya utawawezesha wanafunzi kupata muda na nafasi ya kujiandaa na mitihani ya majaribio.


"Hatua ambayo chuo imechukua ni nzuri, kwa sababu njia hii itamsaidia mwanafunzi kukuza uelewa wake badala ya kutegemea kufanyiwa majaribio na mwenzake", alisema.
Mbwette alifafanua kwamba, wanafunzi waliowengi wamekuwa wakifanyiwa mazoezi na wanafunzi wengine kwasababu ya kuwa na kazi nyingi ambazo zinawafanya washindwe kumudu kufanya majaribio yanayotolewa na chuo.


" Hatua hii itasaidia kwani walimu walio wengi hawasahihishi mitihani kwa muda muafaka, baadhi yao wanasahihisha mitihani mingi bila kujali ubora kwa ajili ya kulipwa fedha nyingi" alisema Mbwette.
Hata hivyo, alifafanua kwamba bajeti ya fedha iliyotolewa na serikali mwaka huu ni ndogo haiwezi kukidhi mahitaji yote ya chuo hivyo bado wanaendelea kufanya jitihada za kuweza kupata fedha za kutosha ili kuboresha elimu ya juu katika chuo hicho.


"Tunaishukuru serikali kwa kukubali kutuongezea wanataaluma ambao watasaidia kwa kiasi kikubwa kufundisha na kufanya chuo kuendelea kuongeza idadi ya wanafunzi, " aliongeza.
Kwa upande wa wanafunzi, walisema wamefurahishwa na hatua iliyochukuliwa na viongozi wa chuo kwa kubadili mfumo ambao ulikuwa ukiwabana, hivyo mfumo huo mpya utatoa nafasi kwa kila mwanafunzi kufanya mtihani kwa nafasi.
Mwanafunzi wa mwaka wa tatu Happy Mbile, alisema mfumo wa awali haukuwa mzuri kwasababu wanafunzi wengi hawakuweza kuonyesha uwezo wao, kwakukosa mda wa kufanya majaribio wenyewe, kulingana na kazi nyingi hasa kwa wale wanaofanya kazi maofisini.

No comments:

Post a Comment