Wednesday, October 28, 2009

Tiketi Simba, Yanga kuanzia Sh5,000 hadi Sh60,000

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limetangaza viingilio baina ya watani wa jadi, Simba na Yanga ambapo kiingilio cha chini kitakuwa shilingi 5000 na kile cha juu kikiwa shilingi 60,000.

Mchezo huo unaosubiriwa na mashabiki wengi unatarajia kufanyika Jumamosi katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambapo mwamuzi wa pambano hilo atakuwa Oden Mbaga.
Katibu mkuu wa TFF, Fredrick Mwakalebela alisema jana kuwa tiketi kwa ajili ya mchezo huo zitaanza kuuzwa leo katika vituo mbalimbali jijini Dar es Salaam ili kuondoa msongamano siku ya pambano hilo na kusema siku hiyo tiketi hazitauzwa.

Kuhusu mpangilio wa viti, Mwakalebela alisema viti vya kijani mzunguko, kiingilio kitakuwa 5,000,viti vya kijani mzunguko 7,000, orange 10,000, orange VIP 20,000, VIP C, 30,000, VIP B 50,000 na VIP A 60,000.

Mbali na viingilio hivyo, Mwakalebela aliwataka mashabiki wa timu hizo kuwa watulivu wakati wa mchezo huo na kuondoa dhana potofu ya ushirikina pamoja na kuwataka kuwa makini kila wanaponunua tiketi ili kukwepa udanganyifu na tiketi feki.

Nao makatibu wa klabu hizo, Mwina Kaduguda wa Simba na Lawrence Mwalusako wameeleza wao hawana la kusema kuhusiana na matokeo ya mchezo huo, hivyo kuwaachia makocha wao pamoja na manahodha wa timu hizo kwani wao ndio wanao uwezo wa kuelezea jinsi walivyojipanga.

Alisema ili kuondoa msongamano siku ya pambano tiketi hazitauzwa, hivyo kuwataka mashabiki na wapenzi wa mchezo huo kununua tiketi hizo mapema ili kuondoa vurugu.

"Tunawashauri mashabiki wanunue tiketi zao mapema kwani siku ya mchezo hatutaruhusu tiketi kuuzwa kwani chanzo cha vurugu ni ucheleweshaji wa tiketi na hivyo ili kukwepa matatizo kama hayo, leo tutaanza kuuza tiketi mpaka Ijumaa jioni ,"alisema Mwakalebela.

No comments:

Post a Comment