Saturday, January 30, 2010

Rais Kikwete anapodai kuwa nchi hii ni maskini!

Rais Kikwete akiwa safarini kwenda Davos, alisimama Libya na kukutana na Ghaddafi na kumpa shukrani kwa msaada uliotolewa na Libya wa kujenga nyumba kwa familia zilizoathirika kwa mafuriko.
Katika hotuba yake, Rais Kikwete alisema yafuatayo ambayo nayanukuu na kuyajengea hoja ya yeye kuudanganya umma!

Nanukuu gazeti.

Rais alisema mafuriko hayo yaliyotokana na mito miwili, ukiwamo Mto Mkondoa kuacha njia za asili na kubomoa kingo, yameharibu mno miundombinu ya barabara na reli kiasi kwamba Serikali ya Tanzania inahitaji kiasi cha dola za Marekani milioni 15 (zaidi ya Sh bilioni 15) kukarabati miundombinu hiyo.

“Ni hasara kubwa kwetu. Kiasi cha dola za Marekani milioni 15 ni nyingi kwa nchi masikini kama Tanzania lakini tumeamua kuwa ukarabati huo utakuwa umekamilika katika muda mfupi”.

Rais anadai Taifa letu ni masikini sana na dola milioni 15 ni nyingi sana!

Kweli dola Milioni 15 ni nyingi hasa zikitumika kwa matumizi yasiyo ya msingi au kipaumbele mbayo ni jambo la kawaida sana kwa Serikali ya Tanzania kutumia fedha kwa mambo yasiyo ya msingi au kipaumbele kwa Taifa zima.

Hata kama fedha hizi zingekuwa ni za mtu, shirika au Taasisi binafsi, inapofikia kuwa fedha zinatumika kwa minajili ya kuwa zipo zitumike, swali linakuja, iweje kama Taifa tuendelee kudai sisi ni masikini?

Kwa nini Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anaendeleza ulaghai, udanganyifu na kutukuza umasikini na unyonge kwa kudai eti nchi ni masikini hatuwezi kuwa na Dola milioni 15 na kuzitumia kwa vitu vya muhimu?
Labda nitumie Jedwali hili kuonyesha ni vipi kauli ya Rais ni ya kizandiki na kinafiki!

1. Benki Kuu imejenga na kukarabati nyumba nne kwa ajili ya Gavana na manaibu wake. Jumla ya gharama zote ni karibu Shilingi Billioni 6 ambazo ni sawa na Dola Millioni 5 ambayo ni asilimia 30 ya Dola Milioni 15.

2. Nyumba ya Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, shirika la umma linalokabiliwa na matatizo ya kifedha kuipatia Tanzania umeme wa kutosha, imegharimu si chini ya Shilingi Bilioni 1.5 ambazo ni sawa na Dola Milioni 1 na ni asilimia 7 ya Dola Milioni 15 zinazohitajika kujenga hii barabara iliyoharibiwa na mafuriko.

3. Chama Cha Mapinduzi, kimetumia takribani kati ya Shilingi Billioni 9 na Bilioni 14 kununua magari 200 kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Taifa wa mwaka huu 2010. Magari haya kutoka Japani ambayo nayapa makadirio kutokana na bei za International Motor Mart au Toyota Motors of Tanzania ambazo kwa magari ya Toyota kati ya Rav4 na Land Cruiser VX yana bei ya chini bila kodi na ushuru kati ya Dola 35000 na Dola 55000. Hivyo iwe kwa kadirio la chini la Shilingi Bilioni 9 ambayo ni sawa na Dola Milioni 7 ambayo ni asilimia 47 ya dola milioni 15.

Kwa mifano hiyo mitatu ya matumizi ya Taasisi na Mashirika yanayohusiana na Serikali ya Tanzania, ni dhati kuwa Tanzania ina uwezo wa kujitegemea na hizo dola milioni 15 si nyingi sana kiasi cha kutangazia umma na dunia kuwa eti sisi ni masikini! Ukichukua matumizo yote ya hizi taasisi tatu tuu, unakuta kuwa tayari Tanzania dola Milioni 13 ambazo ni asilimia 86 ya dola Milioni 15 zinazohitajika kujenga upya barabara na reli huko Morogoro!

Jana katika hotuba yake kwa Bunge la Marekani, Rais Barack Obama aligusia suala la matumizi ya lazima na umuhimu wa Serikali ya Marekani kufunga mkanda na kuachana matumizi yasiyo ya busara na ya holela.

Je Rais Kikwete baada ya miaka yako minne ya kuwa madarakani:

a. umefanya nini kupunguza deni la Taifa?

b. umefanya nini kupunguza matumizi ya Serikali?

c. umefanya nini kuondokana na umasikini?

No comments:

Post a Comment